Saturday, December 31, 2005

KIKWETE ASEMA HALI YA KISIASA ZANZIBAR INAHITAJI MJADALA WA KITAIFA

Rais mteule wa jamhuri ya muungano wa Tanzania bwana Jakaya kikwete jana kwa mara ya kwanza alilihutubia bunge,ikiwa ni siku mbili baada ya kupatikana kwa spika wa bunge hilo na siku moja baada ya uteuzi alioufanya wa ndugu Edward Ngoyai Lowassa kuthibitishwa na bunge kua waziri mkuu wa tisa wa jamuhuri hii ya Tanzania.

Ikiwa kama ni hotuba ya kutoa dira ya serikali yake ya awamu ya nne,mambo mengi aliyazungumzia kwa kina kwa takribani masaa mawili lakini mpasuko wa kisiasa uliopo Zanzibar umeonekana kuchukua uzito mkubwa na kua gumzo katika mitaa mbalimbali ya visiwa hivi ambavyo mchakato wa kisiasa umekua na matatizo makubwa bila kupewa uzito unaostahili.

Kumbukumbu zangu zinanisukuma kusema kua ukiacha mwalimu Nyerere,Jakaya kikwete anakua kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu kuzungumzia suala hilo hadharani ambalo linaonyesha kumkera kama si kumkatisha tamaa kwani halitoi muelekeo mwema kwani hali ya chuki inayoendelea kujengeka katika misingi ya Upemba na Uunguja inazidi kuota mizizi kama si kushamiri.

Inawezekana Kikwete amehamasika kupasua jipu hili kufuatia muendelezo wa matokeo ya uchaguzi yanayoendelea kugawa visiwa hivi katikati.Chama tawala(CCM) hakikuambulia hata kiti kimoja katika kisiwa cha pemba ambacho kinaaminika kua ni ngome kuu ya chama cha CUF,huku CCM ikijizolea viti vyote vya Unguja isipokua katika jimbo la mji mkongwe ambalo wapinzani wanaonekan kujizatiti.Nikiwa katika mizunguko yangu ya kawaida katika mitaa ya mji huo mkongwe leo nimeshuhuda makundi mbalimbali ya watu wakijadili hotuba hiyo huku wengi wakijiuliza ikiwa mfupo uliomshinda Mwinyi na Mkapa yeye(kikwete)atauweza???

Naamini kabisa kua haiitaji viongozi wetu kua na shahada za chuo kikuu ili kubaini uzito wa tatizo lililopo visiwani hapa isipokua ushabiki wa kisiasa ndio unawaponza kuchukua hatua za haraka kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili ambalo ni kama bomu linalosubiri mda kulipuka.Cha ajabu ni viongozi hawa kuchukulia mpasuko huo kama silaha ya wao kujijengea umaarufu wa kisiasa na hata kuendelea kuungwa mkono na wanachama wao.

Nimekua nikijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu sawia,Kwanini watu wafike mahali hadi kushindwa kumpangisha mtu nyumba ya kulala kutokana na chuki zilizojengeka katika hali ya upemba na uunguja?Kwanini watu wasusiane maiti kutokana utofauti wa asili zao?Kwanini watu waendelee kupiga kura za chuki bila kuzingatia uwezo wa wagombea wanaowapigia?Kwanini watu waendelee kutofautishana kwa sura na kunyoosheana vidole vya uunguja na upemba?

Fursa aliyoahidi kuitoa Kikwete kujadili mustakabli wa kisiasa katika visiwa hivi, naichukulia kama tunu ya wanablog kuanza kuelekeza fikra zao katika kutoa nafasi ya TAFAKURI makini zinazozingatia suluhisho zaidi ya kuendelea kuhoji matatizo yaliyopo.Nataka tuichukulie nafasi hii kulifanyia jambo taifa letu jambo la neema na matumaini kwa vizazi vijavyo.

Wednesday, December 28, 2005

KWAHERI MSEKWA

Nafuraha kwa moyoni, tena isio kifani
Babu msekwa kuagani,bungeni tena haonekani
Njema safari nakutakiani,maisha mapya uraiani
Kwaheri kwaheri babu yetu,mda wako tamatini!

Ulianza miaka ya sitini,ukakomea majuzini
Ulitumika vya kutoshani,kwa mema na mabayani
Takrima ulihalalishani,mungu sasa akulipani
Kwaheri kwaheri babu yetu,mda wako tamatini!

Ulidhani wahitajikani,kumbe pekee ulijidhani
Nafasi tena haipatikani,fikra zetu kuchezeani
Ukerewe sasa urudini,ukafuge au kulimani
Kwaheri kwaheri babu yetu,mda wako tamatini!

Kasi mpya imekuzoani,kwa pua ukaangukiani
Ulizani ni matani,ukajidai kung'ang'aniani
Ona sasa yalokupatani,kamwe huwezi kusahau
Kwaheri kwaheri babu yetu,mda wako tamatini!

Kura nyingi ulizopitwani,ni ishara muhimu fikrani
Siku nyingi walikuchokani,walisubiri mda ufikeni
Sasa yametimiani,kwa aibu kuu waondokani
Kwaheri kwaheri babu yetu,mda wako tamatini!

Mongella ulimsulubuni,bila huruma kumwoneani
Wenzake sasa wakurudini, wakukana kama pilato
Maanani wamekutoani,wakaona hustahilini
Kwaheri kwaheri babu yetu,mda wako tamatini!

Nje ya dimba nawe ukaeni,uangalie ya uwanjani
Uwanja wa siasani,ndo mimi nazungumziani
Ukemee na ukosoeni,kama u jasiri na makini
Kwaheri kwaheri babu yetu,mda wako tamatini!
KASI MPYA YAZIDI KUPINDUA VIGOGO CCM-SASA NI ZAMU YA BABU MSEKWA, AANGUKIA PUA.

Ni punde tu nimetoka kuangalia kinyang’anyiro cha uspika wa bunge letu tukufu na ningependa kuwashirikisha matokeo hayo na changamoto aliyoitoa Spika mpya aliyechaguliwa Mheshimiwa Samwell Sitta.

Hakuna shaka kua ushindi wake ulitabiriwa na wengi ila tofauti ya kura alizompita mpinzani wake wa karibu bwana Msekwa ni kielelezo kingine kilicho wazi kua tayari ndugu msekwa na naibu wake walikua hawana mvuto wowote katika bunge lililopita na kitu kilichokua kinasubiriwa ni muda ufike na hatimaye kuwaaga rasmi tena kwa aibu iliyo kuu.Spika mteule amepata kura 217 huku bwana Msekwa akiambulia kura 57 na aliyekua naibu wake amefanikiwa kupata kura yake pekee, yaani kura moja.

Mheshimiwa spika mteule anayejiita “THE MAN OF STANDARDS AND SPEED” ameanza kwa kutoa onyo kali kwa mawaziri watakaoteuliwa kua wajiandae na mijadala mikali itakayozingatia na kuweka mbele maslahi ya taifa kwani wakati wa mzaha umekwisha na kilichobaki ni kusogeza gurudumu la maendeleo kwa Ari mpya,kasi mpya na nguvu mpya “Majibu yasiyojitosheleza hayatavumiliwa na bunge hili” nimemnukuu mheshimiwa spika akiwasihi Mawaziri wateule wajiandae.Yetu macho kwani tumewazoea kwa maneno matamu na utendaji sifuri.

Nafikiri wanablog mnaweza mkazua maswali mengi katika hili,Je bunge lililopita lilikua ni la mzaha siyo? Je msekwa alikua hatoi nafasi kwa ajili ya mijadala hiyo?Je bunge lilikua limepoteza imani kwa Msekwa na Akukweti kwa kiasi hicho?Je falsafa ya ari mpya inataka sura ngeni?Lakini mbona Sitta si mgeni katika System?

Labda nimalizie kwa kutoa wito kwa mheshimiwa msekwa kwasasa ajikite zaidi katika masomo yake ya shahada ya kwanza ya sheria katika chuo kikuu huria cha Tanzania angalau aweze kusajiliwa kama wakili wa kujitegemea ili awasaidie raia kama nia yake kweli ni utumishi!

Tuesday, December 27, 2005

VITA YA KIFIKRA

Ulingoni naingia,hoja kutoani
Africa yangamia,tuingie vitani
Viongozi hatarini,bongo zao usingizini
Hima hima jikazeni,mda hausubirini!

Fikra chakavu nazungumzia,zilizochoka chambua
Uzandiki ndo umezijaa,zisizojali raia
Kila siku kutuhadaa,na hadith zisizoisha
Hima hima jikazeni,mda hausubirini!

Makene twasubiria,mstari wa mbele jitokeze
Ndesanjo nawe fatia,ili wengine wajitokeze
Hali sasa yachefua,ujinga tutokomeze
Hima hima jikazeni,mda hausubirini!

Tusikate tamaa,daima mbele tusonge
Vizazi kuokoa,fikra zao tuzijenge
Rai nazidi toa,wanablog wajiunge
Hima hima jikazeni,mda hausubirini!

Fikra chambuzi ndo silaha,mimi nasisitiza
Hakuna msamaha,tutaotoa kwa bongolala
Wote tuangamize,vionngozi ndo nazungumzia
Hima hima jikazeni,mda hausubirini!

ALUTA CONTINUE!!!!!!!!!!
NB:Mwalimu makene nakaribisha masahihisho na maoni katika masuala ya vina na mizani.

Thursday, December 22, 2005

ANAYEJIITA MUUMINI WA DEMOKRASIA TANZANIA AANZA KULA MATAPISHI YAKE!
Ukweli na umakini wa utekelezaji ahadi ziltolewazo ni miongoni mwa misingi mikuu ya demokrasia.Ni katika mtazamo huo umenifanya kujenga desturi ya kua na hofu pindi nionapo mtu anaenda kinyume na kile alichoamini,na baya zaidi mtu aliyejijengea heshima na sifa katika jamii husika.

Mwaka 2000,Spika anayemaliza mda wake Mh. MSEKWA alitamka hadharani kua hatagombea tena kiti hicho baada ya kulitumikia bunge kwa takriban muongo mmoja kwasasa na badala yake ataachia wenye mawazo na fikra mpya wachukue hatamu. Sitaki kuamini kua miaka mitano ni mingi sana kiasi cha kumfanya mtu asahau aliyoyasema.

Mh. huyu muumini(Msekwa) ameibuka ghafla na kuweka wazi kua amebadili nia yake ya kustaafu na kutangaza kuchukua fomu kwa ajili ya kutetea kiti hicho.Katika hali ya kustaajabisha ni pale msekwa alivyoonyesha kukerwa na maswali ya mtangazaji wa BBC aliyekua anahoji sababu za yeye kuendelea kung'ang'ania hicho.Mhesimiwa alianza kujibu kwa kuhamaki na kunga'ka kana kwamba mtangazaji yule hakupaswa kumuuliza maswali hayo.

Hii tabia inaonyesha kuanza kuota mizizi baada ya mwaka 1995 Komandoo Salmin Amour,aliyekua rais wa Zanzibar kufika mbali hadi kutaka kubadili katiba ili aendelee kubaki madarakani na bila aibu wiki iliyopita alipokua akihojiwa akasisitiza nia yake aliyokua nayo kipindi kile kwa kisingizio kua wananchi walikua bado wanamuhitaji kama anavyojaribu kutueleza Msekwa kua wabunge walimuomba asing'atuke!

Binafsi naamini kua bunge letu limejaa vipaji vya kila aina vinavyoweza kuijaza nafasi hiyo bila matatizo.Ni jambo la heri kua siku hizi mtu binafsi anaweza kuomba nafasi hiyo jambo linalopanua wigo wa kuibuka kwa vipaji vya raia wa kawaida kuiomba nafasi hiyo.HII NI CHANGAMOTO KWENU mh. NDESANJO NA MAKENE mjitokeze na kuwatoa watanzania kimasomaso kwani nahisi waheshimiwa wa aina ya msekwa ni wale walio na hofu ya kurudi uraiani na kuishi maisha ya kawaida kama tuishiyo sisi.

Thursday, December 15, 2005

ISHARA YA USHINDI WA CUF KATIKA JIMBO LA MJI MKONGWE.
Ni kama masaa mawili tu yamepita tangu alipotangazwa MAALIM SANYA kua ndo mshindi wa kiti cha ubunge katika jimbo la mji mkongwe.Wafuasi wa chama cha CUF wlilipuka kwa shangwe kuu huku wakichukua tahadhari kubwa wakati wa hekaheaka zao za kushangilia ushindi kwani vikosi vya usalama vimetapakaa kila kona za mji huo uliozoeleka kua na pilika nyingi wakati wa mchana.

Tunaweza kusema kua ni kama kiini macho kwa chama tawala tawala kwani watakua hawaamini nini kimetokea licha ya kutumia nguvu kubwa katika harakati zake za kukomboa jimbo hilo lililopo mikononi mwa wapinzani tangu mwaka 1995.Tangu jana asubuhi kumekuwepo na lawama za kupandikizwa mamluki wakiwa katika sare za kiusalama kwa ajili ya upigaji kura na hadi sasa hakuna ufafanuzi wa kina uliotolewa na Tume ya uchaguzi ya ZEC.

Nikiwa katika harakati zangu za kuelekea eneo maarufu la darajani kama kiunganishi cha mji huo mkongwe niliponea chipuchupu kutiwa ndani ya wana usalama waliokua wakiranda kila kona za njia ya mji huo wakiwa katika sare zao na silaha kana kwamba wamesikia habari za magaidi kutaka kulipua eneo la bandari lililopo mkabala na mji huo kumbe ni harakati za kuweka mambo sawa kabla ya kutangazwa yale matokeo yasiyotarajiwa kwa upande wao.

Ushindi huu unafungua ukurasa mpya kwa wachambuzi wa masuala ya siasa za zanzibar kwani mengi yameshaanza kusemwa juu ya ushindi huo wa chama cha CUF kua ni kielelezo cha ushindi mkubwa walioporwa october 30.Ushindi huu wa chama cha CUF unakuja huku kukiwa na matukio kadhaa ya kutisha yaliyotokea jana baada ya wafuasi wawili wa CUF kupigwa risasi sehemu za siri na mwimgine kuchomwa kisu cha tumbo.

Hadi napoandika makala hii mji wa zanzibar katika jimbo la mji mkongwe umezizima kwa furaha huku wananchi wakionyesha tabasamu licha ya kudhibitiwa na vikosi vya kiusalama wanaofanya watu waamini kua ushindi huo wa CUF ni kama dhambi ya mauti kwa chama tawala.