Monday, March 27, 2006

HATMA YA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA NA UVAAJI WA SARE ZA KISIASA SEHEMU ZA KAZI ZANZIBAR.

Mojawapo ya mambo ya msingi katika utoaji wa huduma za kijamii ni kutobagua watu katika misingi ya kidini,itikadi za kisiasa na makabila.Siasa za Zanzibar kama mjuavyo ziko tofauti sana na sehemu nyingine za Tanzania kwani kila kitu kimekua kikipewa tafsiri nyeti ya kisiasa hata kama kikiwa chema kiasi gani.

Nilishawahi kuandika katika gazeti tando hili juu ya uhasama uliokuwepo kati ya watu wa pande mbili hizi za Unguja na Pemba katika masuala mbalimbali ya kijamii kama vile kuzikana na hata katika biashara.Watu walikua wakisusia kuzika wafu kwasababu tu huyo ni MUUNGUJA au MPEMBA!au kununua bidhaa sokoni kutoka kwa mtu ambaye anatoka pande nyingine ya kisiwa hiki.

Kwa watu ambao wako nje ya kisiwa hiki wanaweza kudhani hali sasa ni shwari tangu uchaguzi mkuu ulipomalizika mwaka jana,La hasha! kwani bado watu wako katika sherehe za ushindi na maombolezo ya kushindwa katika kinyang’anyiro kilichopita.Huku tukiwa bado tunasubiri kwa hofu nini matokeo ya kauli ya katibu mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha CUF aliyoitoa juu ya mustakabali wa hali ya kisiasa Zanzibar ambayo alitamka wazi kua iko mikononi mwa viongozi wakuu wa tano(5) wa chama hicho nimeona ni busara kulisemea lile ambalo kwa namna moja au nyingine linaonekana kuchochea uahasama wa makundi haya mawili.

Utumishi wa umma unaongozwa na maadili katika utoaji huduma kwa wanajamii kama nilivyosema hapo awali bila ubaguzi wa aina yoyote ile iwayo.Lakini ni jambo la kushtukiza na kutia wasiwasi pale unapoona watumishi muhimu wa umma wakiwa katika sare za vyama vyao vya kisiasa katika kazi ambazo hazihitaji ushabiki wa aina yoyote ile wa kisiasa.Hivi kama mtu alikua anaweza kukataa kumzika mwenzake eti kwasababu ya tofauti zao kisiasa,JE chuki hizo haziwezi kuendelezwa hata katika huduma za afya,elimu na nyinginezo???

Kuna umuhimu gani kwa mtu kuvaa kofia,shati,kanga na beji ya chma chake wakati akijua wazi haileti picha nzuri kwa watu wa upande mwingine.Ushabiki kama huu unaoibua na kuchochea jazba za kisiasa kwanini ziendelezwe huku tukijua wazi hazina muelekeo au mwisho mzuri????Nilishawahi kusikia naibu waziri kiongozi akikemea tabia hiyo wakati wa ziara yake aligusia jambo hilo lakini nadhani ushabiki wa kisiasa walionao viongozi unakwamisha utekelezaji wake.

Haya ni masuala ambayo yakiangaliwa kwa juu juu yanaweza yasionekana kua na madhara,lakini kwa kuzingatia historia ya uhasama wa kisiasa inayoendelea kujikita katika kisiwa hichi,basi ni wazi kua hayo si masuala ya kufumbia macho hata kidogo na ni vyema viongozi husika kuchukua hatua zinazostahili kukomesha hali hii.

Monday, March 20, 2006

SUALA LA AJIRA TANZANIA NA FALSAFA YA TECHNICAL KNOW WHO

Tatizo la ajira nchini mwetu liko wazi sana kwa mtu yeyote yule.Hata wale ndugu zangu waliopo nchi za watu nao pia hili wanalitambua fika.Na kuna uwezekano mkubwa kua wote waliopo huko ughaibuni si kutokana na masomo tu,bali pia katika harakati zao za kulipatia ufumbuzi tatizo hili baada ya kukumbana na kero mbalimbali walipokua wakitafuta mahali pa kujipatia riziki baada ya kazi ngumu ya kuperuzi makaratasi shuleni hadi kufikia kilele cha awali cha safari ndefu ya elimu kama vile kutunukiwa shahada ya kwanza au stashahada.

Serikali imekua ikisisitiza kutiliwa mkazo ukuaji wa sekta binafsi kama njia mbadala ya kulitafutia ufumbuzi tatizo la ukosefu wa ajira kwa wananchi wake.Hili bila shaka ni jambo la heri kabisa.Lakini sidhani kama idara mbalimbali za ajira za serikali na sheria zilizopo zinaenda na wakati ili kuhakikisha mambo katika sekta binafsi yanaenda sawa ili kuepukana na matatizo kama vile ya kuajiri watu wasio na uwezo au bila kuzingatia taratibu zilizopo za ajira.

Naandika waraka huu baada ya kupokea malalimiko kutoka kwa rafiki wa karibu wa MAKENE (ambaye ni Binti) juu ya madhila yanayomsibu katika kampuni moja ya binafsi.Na cha kutia hudhuni zaidi ni jambo hili kutokea katika kampuni ya habari ambayo wengi wetu tungetegemea iwe mstari wa mbele katika kulipigia kelele jambo hili.

Suala la ubinafsi,udugu na unani katika sekta ya ajira kwakweli linatia kichefuchefu na liko katika sura mbili nizionazo kwa harakaharaka.Ya kwanza ni ile inayohusu utaratibu mzima wa kumuajiri mtu katika nafasi Fulani na la pili ni lile la upendeleo ulio wazi kazini unaotokana na kujuana kikabila,kindugu au kihusiano na zaidi ni katika masuala ya mapenzi.Nafikiri la mwisho ndilo linaloota mizizi zaidi kwani matokeo yake ni kuharibika kwa kazi.

Nani atabisha kua asilimia kubwa ya wakuu wa idara mbalimbali wana uhusiano wa kimapenzi na makatibu muhtasi wao?Nani atajifanya kusema kua hajui matokeo ya uhusiano huo kua ni kuharibika kwa kazi na kukua kwa dharau kati ya makatibu hao na waajiriwa wengine?Nani ambaye hatambui kua kwasasa asilimia kubwa ya makatibu muhtasi wa wakubwa katika makampuni binafsi ni wale wasiokua na sifa na elimu stahiki kushika nafasi hizo?Nani ambaye hajui kua hawa makatibu muhtasi wamekua na sauti ndani ya mashirika au makampuni binafsi kuliko hata hao wakubwa zao?

Ni majuzi tu nilivyokua Arusha nikimalizia masomo yangu nikiwa katika harakati zangu za kutafuta ajira nikapeleka maombi ya kazi katika shirika moja Mkoani Arusha nikiwa na uhakika wa kuilamba hiyo nafasi.Nikiwa natoka mlangoni mwa ofisi hiyo nikakutana na rafiki yangu tuliyekua tunasoma pamoja shule ya msingi.Katika maongezi yetu nikamueleza lengo la mimi kwenda pale ofisini lakini nilipata hofu nilipomuona ameshtuka na kutikisa kichwa kuonyesha masikitiko yake na ndipo nilipoona kuna umuhimu wa kuhoji kulikoni.Jawabu likawa “huyo Katibu mushtasi wao ana tabia ya kuzichana au kuzichoma moto barua za maombi ya kazi za watu na kutafuta vihiyo wenzake ambao ni jamaa zake kwani uhakika wa wao kupata ajira ni mkubwa kutokana na bosi wao kumuweka kiganjani”!!!!!
Kama nilivyosema hapo juu kuhusu rafiki wa karibu wa Makene aliponipa taarifa za kunyanyaswa na kusengenywa na katibu muhtasi wao nimeona ni busara kushirikishana tena huu uozo ambao wengi wetu tumekua tukishuhudia na tuweze kuchangia juu ya nini kifanyike ili tuokee hali katika hizi idara zianazotegemewa kua kimbilio la watu kujipatia ajira.Nimeambiwa kua imekua ni desturi kwa makatibu muhtasi hao kuwasema kwa mafumbo yanayoshadahishwa na tungo za pwani(Taarabu) wale wafanyakazi wenzao ambao wana chuki binafsi ilhali wakuu wa idara na mashirika husika wanafumbia macho vitendo kama hivi vya kishenzi.Hivi kuna uhalali upi kwa mtu aliyemaliza darasa la saba na asiye na uzoefu hata wa mwaka mmoja kulipwa mshahara maradufu zaidi ya yule mwenye shahada zaidi ya moja na anayeshika nafasi nyeti katika shirika husika????

Hali sasa inazidi kua mbaya kupita maelezo.Kila anayeona tangazo la kazi mahali,kitu cha kwanza anachofanya ni kutafiti na kujua kama ana ndugu,jamaa au rafiki katika sehemu husika ya ajira tarajiwa.Huu utaratibu ndo umekua unazidi kukandamiza wenzangu na mimi wanaotokea TANDAHIMBA kama akina makene kushindwa kupata ajira pindi wamalizapo masomo yao.Hivi sasa vyeti vya taaluma vinakua kigezo cha mwisho kuzingatiwa na badala yake kujuana ndo kumeshika hatamu zaidi.Vikwazo vinakua vingi haswa kwa dada zetu wanaolazimishwa kuziweka taaluma zao kapuni au kwenye pochi na badala yake kutumia miili yake ili kujihakikishia nafasi zilizotangazwa na ambazo nionazo mimi ni kama haki zao.

Nionavyo mimi,ili maisha bora yapatikane kwa kila Mtanzania nadhani utaratibu mzima wa ajira unapaswa kutazamwa upya.AU MWASEMAJE WAKEREKETWA WENZANGU WA GAZETI TANDO?????????????