Kikwete chukua tahadhari wananchi wanakuasi
Uasi katika kamusi ya Kiswahili umepewa tafsiri ya tendo la uvunjaji wa kanuni, sheria au amri na pia imeelezwa kuwa ni tendo lolote la uhalifu unaolenga kuvuruga amani katika nchi au jamii husika. Nimekua nikitafakari matukio ya hivi karibuni ya wananchi kukaidi amri au maagaizo ya serikali bila uoga wowote na ujasiri huo umekua ukiongezeka kwa kasi ya ajabu.
Mijadala mikali imekua ikiendelea kuibuka kila kukicha kupinga hoja au maelekezo yanayotolewa na watendaji wakuu wa serikali. Kauli zenye jazba, hamaki na zilizosheheni matusi ya nguoni zimekua zikielekezwa kwa watu muhimu waliopewa dhamana ya kuboresha maisha ya Watanzania maskini ambao hupigana usiku na mchana kutafuta kipato kilicho chini ya wastani wa dola moja ili kuweza kujikimu maisha yao na watoto wao.
Si lengo langu kujitumbukiza katika mijadala hiyo, bali kutaka kufikisha ujumbe kwa watawala wetu hasa Rais ambaye ndo nahodha wa meli yetu iitwayo ‘MV Tanzania’. Ujumbe wa kwanza ni kuwa watawala watambue kwamba Watanzania wa sasa si wale wa miaka ishirini iliyopita waliokuwa wanatambulika kama watu wa ndiyo mzee!
Sio wale waliokuwa wanadhani kumpinga kiongozi wao ni utovu wa nidhamu!Bali sasa wanajua ni wajibu na haki yao ya msingi kuhoji pale ambapo wanaona mambo hayaendi sawa sawia.
Mfululizo wa migomo unaondela katika nchi hii si jambo jema na la kutia matumaini bali ingetosha kuwakosesha usingizi watu waliopewa dhamana kusimamia utekelezaji katika idara au sekta husika ‘Respective portifolio’. Nilianza kuingiwa hofu pale wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walipoamua kujitokeza barabarani kupinga ongezeko la nauli huku wakiwa wamebeba mabongo yenye ujumbe wa kejeli kwa viongozi waandamizi wa serikali yetu.
Wafanyakazi katika kila sekta nao hawakamatiki. Inauma sana na kutia mashaka pale unapoona wafanyakazi wa sekta ya afya kila siku malalamiko na vitisho vya kugoma haviishi. Wagonjwa wanaishi kwa hofu kuu na kukata tamaa kwani hawajui ni lini hawa watu wataweka vitendea kazi vyao chini na kusababibisha madhara makubwa.
Nazidi kuwaonea huruma wale ndugu zangu wanaougua shinikizo la damu kwani utulivu wa fikra ambao ni tiba muhimu ni kama haupo katika mazingira hayo ya utoaji huduma. Wakina mama wajawazito nao hofu kila siku inazidi kutanda kwani hawajui kama viumbe vyao walivyoteseka kuvibeba katika matumbo yao wataviona vikiwa hai kwani uhakika wa huduma umetowaka kwa sasa.
Katika utangulizi wa makala hii niliieleza nini maana ya uasi. Neno hili kama nilivyosema limekuwa likihusishwa na uovu unaolenga kuleta machafuko au hali ya vurugu kwa jamii husika.Nikitafakari kwa undani naona kuna mantiki kubwa katika kitendo hiki cha kuasi kama kitakuwa na lengo la kuleta mabadiliko kwenye jamii yenyewe.Natamani sana wananchi waendelee kuasi kwa lengo kuu na la dhati la kubadilisha maisha yao ambayo kwa sasa wanaona na kudai yanaharibiwa au kuchafuliwa na watu waliowapa dhamana ya kuwaongoza.
Kila kona ukipita utasikia usemi huu “Hivi hii nchi ina viongozi kweli” kutoka kwa raia wa kawaida ambao awali hakuna mtu angedhani watu wenye tabaka la chini na walalahoi wangeweza kupata ujasiri wa kuhoji kwa kiwango hicho cha kejeli. Hofu za watu hawa dhidi ya watawala imetoweka, imani waliyokuwa nayo awali nayo imekalia kuti kavu hakika hakuna maneno mbadala ya kusema zaidi ya “Nahodha wetu Kikwete shika usukani wako kwa makini”.
Nilishawahi kuandika makala moja yenye kichwa cha habari “Mheshiwa raisi ukiamua unaweza” na leo ningependa kukuomba urejee makala ile kama ulipata bahati ya kuisoma au hata kuhadithiwa. Nchi hii mheshimiwa rais ni changa sana na watu wa kuitoa hapa ilipo ni Watanzania wenyewe kuchapa kazi bila kuchoka na kwa kwa moyo mkuu na sio wahisani kama ambavyo viongozi wetu wengi wamekuwa wakihubiri kila kukicha.
Serikali imeenda mpango mkubwa kukuza kilimo lakini napatwa na wasiwasi na kasi ya madai ya wadau muhimu katika sekta ya usafiri kama wa reli kutishia kugoma kila siku. Je, mazao yatakayozalishwa yatasafirishwa vipi ikiwa usafiri wa anga umekua unabaki kua historia kwa wakulima wetu wa vijijini?Je, mpango mkubwa wakukuza elimu ya msingi na serikali utafanikiwa vipi ikiwa kila siku walimu wanagoma kutishia kuingia madarasani? Elimu bora itapatikana vipi ikiwa tatizo sugu la usafiri kwa wanafunzi halitapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuwaondelea adha ya hofu wakati wa asubuhi na jioni wakielekea na kutoka mashuleni?
Mheshimiwa raisi kikwete wananchi hawa si wavunjaji wa makusudi wa sheria wala si wendawazimu wa kutaka kupoteza mda pasipo kuchapa kazi bali wanataka sikio litakalosikia na kuwahakikishia kuyapa madai yao uzito unaostahili ili nao wajione ni sehemu ya nchi hii kwani wamekuwa wakivuja jasho jingi ili kuwahudumia wapiga kura wako ambaomda si mrefu utawarudua tena kuwaomba ridhaa ya kuwaongoza.
Sidhani kama itakuwa ni busara pale mwaka 2010 utakaporudi na kuwauliza kwamba wanavaa viatu namba ngapi wakati vipimo ulishavichukua tangu mwaka 2005! Maandamano ya wazee wastaafu wa iliyokua Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kutaka kukuona wewe binafsi ni ishara tosha ya wewe kutambua wasaidizi wako wamepoteza imani kwa wananchi wanaowahudumia. Huo si uasi bali ni chachu ya mabadiliko ya kiutendaji.Naamini wewe ukiaamua unaweza liwe hata kesho na kero hiyo itoweke machoni kwetu. Si busara katika hali ya kawaida kuona wazee wakilia machozi huku wakijigalagaza chini kudai haki yao ya utumishi uliotutaka kwa nchi hii kwa kitambo chote hicho.
Nimekuwa najiuliza iweje watumishi wengine walio katika ngazi za utendajii wanapogeuka mbogo kudai marejesho ya fedha wanazotumia wanapokwenda safari au kucheleweshwa kupewe japo posho zao! Kwa nini wafanye hivi wakati wanakwamisha malipo halali ya wastaafu niliowazungumzia hapo juu ama kutofanikisha maenedeleo ya nchi ambayo inawapa mishahara na nafasi ya kuomba posho na safari kila kukicha?
Kwa nini walimu, madaktari na wengineo wabaki kugoma ili kupata haki yao ya kupandishiwa mishahara huku hali ya maisha ikifahamika wazi kuwa imepanda? Je, taifa hili linatoa haki nyingi kwa kundi la akina ninyi mheshimiwa Rais na kupora haki za watu wa chini ambao wanakilishwa na walimu, madaktari na wafanyakazi wa sekta nyingine?
Wahenga walishasema kuwa, ‘mdharau mwiba mguu huota tende!’ Kwa mantiki hii hatuna budi kuchukua tahadhari kukabiliana na hili vuguvugu la migomo, manung’uniko na kila aina ya ukatishwaji tamaa visigeuke kua vyanzo vya vuruga katika taifa letu ambalo limekua likisifiwa kila mara kwa kudumisha amani tangu uhuru. Kuna usemi mmoja ambao umekuwa ukitawala sana kwa watu wanaopenda kunywa vilevi kuwa “Mpe maskini kileo asahau shida zake”. Mantiki ya usemi huu iko wazi sana na ni wajibu wa viongozi wetu kuufanyia kazi.
Wananchi hawa wanaoasi kila kukicha, hawataki madaraka ya kuongoza nchi hii au nafasi za kisiasa; bali ni haki zao na madai yao ya msingi kusikilizwa na sikio lenye huruma na kuwaondoa katika adha ya maisha haya ya mateso na shida wakati wanadai haki zao. Wanafunzi, walimu, madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine katika sekta za usafirishaji hawana la zaidi mheshimiwa rais zaidi ya kutatuliwa kero zao za madai.
Ili tuijenge nchi hii inapaswa kila mtu atimize wajibu wake katika kila eneo alipo. Hali hii itasaidia kuharakisha jitihada za kuiondoa nchi yetu katika lundo la kero zisizokwisha. Ni wazi kua haya hayatafanikiwa ikiwa kila siku watu wako barabarani wamebeba mabango ya kilio katika kila kazi wanayofanya na kuwakatisha tamaa hata wale wanaojiandaa kuingika katika utumishi wa aina hiyo.
Ukipita vyuo vya Ualimu na Vyuo Vikuu ambapo walimu wanaandaliwa utajua kuwa hali si nzuri na haileti matumaini yoyote na tija katika utendaji kazi. Walimu wanafunzi wamekata tamaa, madaktari wanafunzi wamekata tamaa katika kiwango cha kutisha kiasi kwamba wanajuta kwa nini wamejitumbukiza katika fani ambazo badala ya kuwalipa neema inawalipa kero kuu inayowafanya kujikondoea kama vile wanaishi bila kula au kunywa.
Hii nchi ni yetu sote ila tunatofautiana katika majukumu ya kiutendaji kwa hiyo sioni sababu kwa nini wale waliopewa dhamana ya kuwatimizia mahitaji muhimu na ya msingi wale walio nje washidwe kufanya hivyo kwa hiyo zifanyike jitihada za makusudi kufanyia kazi kwa kasi hizi kero za wananchi ili kuondoa fikra zalizojengeka miongoni mwa Watanzania walio wengi kuwa “nchi hii inajengwa na wenye moyo na kuliwa na wenye meno”. Mungu ibariki Tanzania.
1 comment:
Nice blog and article, thanks for sharing. However want to statement on few common issues, The website taste is great, the articles is in point of fact excellent.
Obat Pelangsing Alami
Post a Comment