TUNAJUA UNA DHAMIRA YA DHATI MHESHIMIWA RAIS; TUNASUBIRI UWEZO WAKO UTAMALAKI
Mheshimiwa Rais,ni miaka miwili na nusu sasa imepita tangu ukamate madaraka ya juu katika nchi hii changa iliyojaliwa kila aina ya rasilimali adhimu lakini bado inasota kwenye dimbwi kuu la umaskini.Nafarijika kua yaliyojiri hivi karibuni yamekupa jawabu ambalo lilikua wazi ulipoulizwa kwanini Tanzania ni nchi maskini wakati ina kila rasilimali muhimu za kuchochea maendeleo kwa kasi na nguvu kubwa.Hilo la BOT ni moja tu mheshimiwa yanayoweza kueleza kwanini juhudi zako na zetu sote hazizai na hazionyeshi matumaini yoyote ya kuzaa matunda.
Mheshimiwa Rais, ni mengi yalisemwa juu yako baada ya kupitishwa na chama chako katika mchakato uliovuta hisia za watu wengi huku tukishuhudia mijadala iliyojengwa katika misingi ya ubaguzi na kishabiki ya urangi, ukabila na uwenzetu. Kuna ambao hatukua na hofu juu ya uwezo wako,dhamira yako na utashi wako katika kutumikia umma huu wa watanzania walioanza kupoteza matumaini baada ya kipindi kirefu cha kuteseka.Hakika uteuzi wako ni kama vile ulihuisha nuru ya mafanikio kwa watanzania kwa kiwango cha juu sana.
Mheshimiwa Rais, wengine walikuhukumu kwa haiba yako!!!eti sura yako nzuri haina mashiko katika siasa za mikikimiki za kibongo!!!Hakika hii ilikua pigo kubwa katika mapambano ya kifikra kwa watanzania.Nikapiga moyo konde kwa kusema mbona hata Clinton alikua na haiba ya kuvutia lakini akaacha historia ya kiutawala licha ya kuandamwa na misukosuko mingi ya vimwana katika ikulu ya marekani!!!Fikra kama hizo hakika hazikua na maana kwa watu wenye akili timamu.
Mheshimiwa Rais, Hotuba yako ya December 30 2005 wakati unazindua bunge ilikua ni hatua muhimu ya kubadili mitazamo hasi juu yako.Hakika matumaini yalihuishwa kwetu sote tuliokua na imani juu yako japo tukikatishwa tamaa na baadhi ya shutuma na fununu zilizoandama uteuzi wako na wasaidizi wako katika kutimiza ilani ya chama chako iliyofanikiwa kushinda kwa mithili ya kishindo cha 'tsunami' kama tulivyoshuhudia wote.
Mheshimiwa Rais, naomba katika makala hii nikufananishe na mpasha mwaidha wa timu(team coach). Wewe ni mtu wa muhimu sana katika kusoma uwezo wa timu yako na kufanya mabadiliko kadha wa kadha ili kujihakikishia ushindi wa timu yako. Haiwezekani kamwe mapenzi yako juu ya wachezaji fulani kukakufanya uache kufanya mabadiliko kwa hofu ya kuharibu uhusiano wako na wachezaji wako ambayo matokeo yake ni wazi kuwa unaweza kupoteza mechi na pia kupoteza imani ya mashabiki wako ambao siku zote huwa na shauku ya kocha wa timu yao kuandaa kikosi cha ushindi ambacho daima kitawaletea furaha.
Mheshimiwa Rais,kauli yako uliyoitoa Dodoma wakati wa kuhutubia bunge bado iko vichwani mwa watanzania wengi na ninadiriki kusema ilikua ni kauli ambayo ilifanya uma wa kitanzania kusema kua "Sasa kazi imeanza".Mimi binafsi nilikua nina shauku sana ya kuona mambo makubwa yakitokea siku za usoni.
Mheshimiwa Rais, je unakumbuka kauli hii "URAIS WANGU SIO WA UBIA NA MTU". Hii ni kauli nzito iliyojengwa katika umakini na udhati mkuu uliyoitoa mbele ya chombo tukufu cha kutunga sheria ambacho ni cha wawakilishi wa watanzania waliokupigia kura huku jua likiwawakia utosini mwao.Ni kweli kabisa wewe ndo mwenye dhamana ya kuongoza timu yako bila kushawishiwa vinginevyo na yoyote yule ambaye ataonyesha kutimiza matakwa yake binafsi kinyume na matarajio ya wengi ambao ni watanzania wenzako.
Mheshimiwa Rais, hivi umeshagundua kua ndani ya timu yako au jeshi lako kuna "Mamluki" wanaofifisha jitihada zako? Nadhani bado utakua unamkumbuka mwanafalsafa mmoja kwa jina la NICOLLO MACHIAVEL.Huyu mtu alipinga sana matumizi ya wanajeshi mamluki au wa kukodi akiamini kabisa hawana uchungu wa kupigania nchi yao kwa dhati kwani wanaongozwa na tamaa ya pesa zaidi kuliko uzalendo.
Mheshimiwa Rais, je umeshafanikiwa kuwatambua watu wa aina aliyoisema mwanafalsafa huyo katika timu yako au jeshi lako ambalo aliyekutangalia alilibatiza jina la askari wa miavuli? Je kama bado, ni ipi nafasi yetu kuwaanika watu hao ili hatua za dhati uzichukue???Naamini hutawabania kama ilivyo kwa orodha ya wafanyabiashara wa unga na majambazi ambao watanzania wenzako waliamua kukuletea kwa nia njema kabisa lakini hadi sasa hatujashuhudia lolote lile au ndo mambo ya subira huvuta heri!!!
Mheshimiwa Rais,hatua za haraka ulizochukua baada ya kuuawa kwa watanzania wenzetu wafanyabiashara wa mahenge kutoka mkoani Morogoro ilikua ni kama mwanzo wa mapambano ya ukweli na dhati dhidi ya ubabaishaji wa watumishi wengi wa umma.Sitaki kuamini na kusema ile ilikua ni nguvu ya soda au uamuzi ule ulifanyika kwa vile ulikua unahusisha dagaa wadogo ambao wasingeweza kutia doa serikali yako kuu iliyoingia na ahadi kibao za matumaini .Hatujakata tamaa bado tunasubiri pengine tutasawazisha kwenye dakika za majeruhi ukizingatia hapa bado tuko mapumziko(Half time).
Mheshimiwa Rais, nilishasema hapo awali na ninarudia tena "Ukiamua uwezo wako utatamalaki". Wewe umepewa mamlaka makubwa sana mheshimiwa rais ili uweze kudhibiti utovu wa nidhamu kwa wasaidizi na wachezaji wako na sioni sababu kwanini ushindwe kutimiza matumaini yetu na matarajio tuliyonayo kwako!!Hili la BALALI ni moja tu ambalo nathubutu kusema ni kama vile umepapasa tu na bado hujaamua kushika. Hakika ukiamua, Tanzania yenye neema, haki na usawa katika mgawanyo wa rasilimali za nchi yetu inawezekana.
Mheshimiwa Rais, hivi unamfahamu huyu jemedari mkuu anajiita "JEETU PATEL".Kama nimekosea herufi za jina lake naomba uniwie radhi kwani huwa mara nyingi sipendi kusoma habari zake kwani zimekua zikinichafua roho na kunikatisha tamaa ya kuishi katika nchi hii hiyo tuliyozoeleshwa kuamini kua imejengwa katika misingi ya usawa na haki. Hivi yeye ni nani katika nchi hii asiyefikiwa na mikono mirefu ya dola na sheria ambayo ina uwezo wa kuwafikia wamachinga na vibaka wadogo waliotapakaa nchi nzima!!Au unataka tuamini kua huyu ni mtume wa mwenyezi mungu asiyepaswa kuhojiwa lolote na mamlaka za kidunia!! Jibu hapa nadhani ni hapana na pengine wewe kwa kimoyomoyo unasema "Dawa yake iko jikoni inachemka". Tunayo imani na wewe mkuu.
Mheshimiwa Rais, kauli yako uliyoitoa wakati wa hotuba yako ya kufunga mwezi wa Januari 2008 ya kutaka kutenganisha siasa na biashara ni ishara ya tumaini jipya linaloendeleza na kudhifirisha umakini wako kiutendaji .Je nia hiyo uliipata siku moja kabla ya kutoa hotuba au ilikua fikrani mwako tangu zamani??Naomba univumilie sana mheshimiwa rais kwa maswali yangu ya uchokozi.Sio utovu wa nidhamu bali ni shauku ya kutaka kujua mambo hasa yanayohusu nchi yangu na viongozi wangu waliokubali kutoa kiasi kidogo cha fedha kugharamia elimu yangu inayonipa ujasiri japo wa kuhoji haya ambayo vinginevyo nisingekua na uwezo wa kuhoji.
Mheshimiwa Rais, mimi nilidhani kabisa kua kauli hii ungeanza kuitekeleza ndani ya chama chako katika uchaguzi mkuu uliopita siku si nyingi ambao kwa hakika unaandaa mazingira ya watu hao kutembea vifua mbele katila ulingo wa siasa za nchini mwetu.Hii ni vita kuu uliyoitangaza na hauna budi kuipigana hadi mwisho wake na kama utaitekeleza kwa vitendo utakua hujachelewa hata kidogo na watanzania wote bila shaka watakua nyuma yako na kukuunga mkono katika jambo hili nyeti.
Mheshimiwa Rais, nafarijika sana na kauli hii ya kutenganisha biashara na siasa kwani imekuja wakati nikiwa bado natafakari kwa kina kauli kama hiyo iliyotolewa na kijana ambaye nadiriki kusema kua alionyesha kiwango cha juu cha umakini na uadilifu katika siasa na utumishi wa uma.Hili nalo nitaliandalia muda wake maalumu ili kulizungumzia kwa kinagaubaga na nikipata nafasi siku nyingine nitakupa muhtasari wa yale tuliyojadili kwa siku ile kwani nadhani yalikua na mantiki kubwa katika mwenendo was siasa za nchi yetu.Ningetamani sana kama ungekua unatenga mda wa kubadilishana mawaidha na kijana huyo mara kwa mara kwani naamini ni hazina kubwa katika siasa za chama chako na taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Rais,nimekua nikikerwa sana na kauli ya "Siasa ni mchezo mchafu" na kama hali hii itaachwa iendelee ni wazi kua hata raia wako wote wanapaswa kuamini kua hata wachezaji wenyewe wa mchezi huo pia ni wachafu!!Sasa mimi sitaki kuamini kua na wewe ni miongoni mwao na kamwe sipaswi niaminishwe hivyo kwani dhamira yako naamini ni safi.Katika hili una jukumu kubwa la kutuonyesha kua sivyo na usikubali hata siku moja watu wasio na ubia na urais wako wakuchafue,tungependa ubaki mweupe kama theluji ili Tanzania uliyotuahidi ionekane.Hakika ukiamua uwezo utatamalaki.
Mheshimiwa Rais, hivi unajua 2010 haiko mbali? Unajua kua siku hiyo utasimama peke yako kuwapigia magoti watanzania wale wale wa 2005? Sasa kwanini ukubali wachezaji wako wakusababishe ushindwe kufika nusu fainali wakati uwezo wa kubadilisha timu ya ushindi unao? Usikubali wananchi wakaja na kauli ya "samaki mmoja akioza….."Hii ni hatari sana mheshimiwa rais mtanzania mwenzangu ambaye ningependa pia uingie katika awamu nyingine ya utawala wa kipindi kingine cha miaka mitano hadi 2015.
Mheshimiwa Rais,Unalo jukumu la kututhibitishia kua utenguzi wa gavana Balali haukufanywa katika misingi ya KUTOLEWA KAFARA.Nakumbuka mwaka 2001 wakati naanza shahada yangu ya kwanza ya siasa na utawala katika chuo kikuu cha Dar Es Salaam,mheshimiwa rais mstaafu wa awamu ya tatu alikuja kuzindua majengo ya hostel za mabibo ambazo kwa kiasi kikubwa zilisaidia kutatua tatizo la malazi kwa wanafunzi.Sisi tulikua watu wa mwanzo kutumia hosteli zile na kila mwanafunzi alikua akisifia mradi ule kwa maneno mafupi sana na yenye kuonyesha imani na viongozi wao.Napenda kuwanukuu "HAKIKA HAYA NI MATUMIZI MAZURI YA FEDHA ZETU".
Mheshimiwa Rais, hivi unajua majengo hayo yaligharimu kiasi gani? Ni shilingi bilioni 16 tu basi.Sasa jaribu kutumia taaluma yako ya MAGAZIJUTO uweze kujua tungekua na majengo kama hayo mangapi kwa fedha alizochota Balali na wenzake ambao bado serikali yako haijaamua kuwaweka bayana il umma wa watanzania wajue japo ni wazi kua itazidi kuwapandisha presha na kuwapa magonjwa ya moyo na kisukari.
Mheshimiwa Rais, ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi katika vyuo vikuu vyetu nchini limezidi kuongeza ukubwa wa tatizo la malazi na sina hakika kama wasaidizi wako katika wizara husika wanakupa uhalisia wa tatizo hili kwani naamini ungeshalitolea tamko kama ilivyo kawaida yako.Siku hizi hosteli za mabibo chumba kimoja wanakaa wanafunzi nane.Hii ni hatari sana kwa afya za vijana wako ambao tunawategemea kama viongozi wetu wa baadae!!!!Tafadhali fanya jitihada turudishiwe hata bilioni 16 katika hizo alizochota balali na wenzake ili tuweze kujenga hostel nyingine kama zile za mabibo ili tupunguze ukubwa wa tatizo hili.
Mheshimiwa Rais,mgongano wa maslahi hasa kwa watumishi wa uma ni kitu hatari sana ambacho kama hakitatafutiwa dawa mapema kinaweza kuiangamiza nchi hii ambayo umedhamiria kuongoza mapambano ya kuikwamua katika umasikini unaoitafuna kwa kipindi kirefu sasa.Tanzania huru bila umaskini inawezekana,TIMIZA WAJIBU WAKO kama ulivyoainisha katika kauli mbiu ya kampeni ya kitaifa ya kupambana na ukimwi.
Mheshimiwa Rais, timu yako ina washambuliaji na viungo hodari sana ambao inakosa ushirikiano kutoka kwa wengine hivyo kushindwa kucheza kama timu.Kuna huyu kiungo wako anaitwa Magufuli, ni hodari kweli kweli ila sehemu ya ukabaji au udhibiti bado butu sana.Hapa nazungumzia hazina ambayo wewe binafsi ulithubutu kuiita roho ya uchumi wa nchi.Kwanini mabadiliko yasianzie hapo mheshimiwa? Au katika hili tutumie ule msemo wa mambo mazuri…na kima ndivyo mheshimiwa rais tutakua hatujachelewa kweli??.Bado tuna imani na wewe na hakika iko siku watumishi wababaishaji watajua wewe ni nani ila tafadhali sana usichelewe kulifanikisha hili mheshimiwa kwani waswahili hao hao waliotoa msemo huo wa mambo mazuri… wanatuonya pia kua ngoja ngoja huumiza matumbo. Wewe ni mtu mzima na makini mheshimiwa rais na unajua hapa namaanisha nini.
Mheshimiwa Rais,kuna suala la EPA(Economic Partnership agreement) au ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi zetu za afrika mashariki na jumuia ya ulaya ambalo lilipata kujadiliwa bungeni ila nasikitika kusema kua majibu yaliyotolewa na mshambuliaji wako hayakukidhi haja bali yalijengwa katika misingi ya ushabiki sana kuliko uhalisia wa jambo lenyewe.Hivi ni yapi mema tunayoweza kusema wenzetu wa nchi za Pacific na carebean wamenufaika nayo na sisi tukashawishika kujiunga katika ushirikiano huo? Nisilaumu sana kwani niligundua baadae kua ufahamu wa wabunge wengi hasa wa chama tawala katika hilo ulikua si wa kuridhisha ndo maana ukimya mwingi ulitawala wakati wa mjadala na kuachiwa viongozi wa upinzani kuteka hoja hiyo ambayo baadae ilihitimishwa bila ushawishi wa kimantiki wa nchi yetu kuingia katika huo ushirikiano.
Mheshimiwa Rais, naomba hilo la EPA nilitafutie mda mwingine ili niweze kumalizia kwa kusisitiza machache.Mosi, endelea kutambua kua sisi watanzania tuna imani kubwa kwako ila tumechoshwa na utendaji wa baadhi ya wasaidizi wako.Mbili, watanzania bado wana shauku kubwa ya kupata undani wa kujua yaliyojiri katika ripoti ya Richmond na kwenye ripoti ya Ernst & Young ya ukaguzi wa mahesabu ya akaunti ya madeni ya nje au kwa kitaalamu External Payment Arears Account (EPA).
Mheshimiwa Rais,hivi ile tovuti ya serikali uliyoisimamia kidete iundwe si ndo ingekua mahali muafaka wa kuanika ripoti hiyo ili kuendeleza falsafa ya uwazi iliyosisitizwa na mkuu aliyekutangulia ambaye ni wazi kua hakufanikiwa kuiishi falsafa yake!Ni kweli iliyo wazi kua kama hilo lingefanyika imani kuu na ushirikiano ulio tukuka ungeupata kutoka kwa watanzania wenzako ambao wengine wamefikia hatua ya kuwaita WADANGANYIKA.Hili mimi silikubali hata kidogo mheshimiwa rais na naomba uniunge mkono katika msimamo wangu huo kutokana na ukweli kua sisi watanzania ni watu makini na tukiamua tunaweza kufanya lolote lile.
Mheshimiwa Rais, kwa leo naomba kuwasilisha hayo machache ambayo pengine kwa maoni ya wengine yanaweza kua kero ila kwa mujibu wa katiba yetu uliyoapa kuilinda na kuitetea inatoa fursa hiyo kwa mtu binafsi kama mimi nilivyofanya kuelezea dukuduku langu a mtazamo wangu juu ya nchi yangu ninayoipenda sana ambayo nina ndoto kua siku moja inaweza kua kama PARADISO.
Mheshimiwa Rais, Natamani sana niendelee kuandika kuhusu bodi ya mikopo ya elimu ya juu ila mda nao unanitupa mkono lakini naahidi kutekeleza hili siku za usoni kwani hili ni eneo jingine ambalo USANII usio na mfano umetawala kwa kiwango cha juu sana.Naahidi siku hiyo nitakusimulia kisa cha kweli cha binti mmoja kutoka katika familia ya kimaskini sana ambaye alikosa haki yake ya msingi ya kuendelea na elimu ya juu kutokana na vigezo vya ajabu vilivyowekwa na bodi hiyo ambayo imekua kama wasanii wa kizazi kipya wa kuonekana wenye luninga kila mara pasipo kua na jipya lenye kutia moyo na tumaini kwa wanafunzi wanaohitaji huduma hiyo.Majibu mepesi mepesi yanayotolewa na wenye dhamana katika wizara husika ni ya kukatisha tamaa na sina maneno mbadala zaidi ya kusema ni kama MSIBA mwingine uliyoipata sekta ya elimu ya juu nchini.
Nakutakia afya njema na kazi njema mheshimiwa rais kwani bila wewe hakika chombo hiki (TANZANIA) kitapigwa na mawimbi na hatimaye kitazama bila kuokoa wahanga hata mmoja.Nia na uwezo unao mheshimiwa rais, sasa kwanini usiviruhusu vitamalaki!!!
Ni mimi raia wako mtiifu,