Tuesday, March 30, 2010

MAJIBU RAHISI YA WANASIASA KATIKA MATATIZO MAGUMU YATAANGIMIZA WANANCHI
Katika makala yangu ya toleo namba ….. kwenye gazeti la rai nilizungumzia ugonjwa wa wanasiasa wetu wa kiafrika hasa wa kitanzania ama kupuuzia utajiri wa kifalsafa,miongozo na maadili ya kiuongozi yaliyosisitizwa na waasisi wetu waliopata kuongoza nchi yetu na bara letu kwa ujumla. Nilijaribu kuhusisha tatizo hilo linaloonekana kuwa kubwa na ama tabia ya viongozi hao kutopenda kusoma au kupuuzia machapisho au hotuba za waasisi na wanafalsasa wetu walioandika mambo mengi mema na muhimu ambayo yanaweza kuwa ni dira muhimu katika uongozi wa uma.

Kwa leo ningependa kurejea maono na onyo alilotoa hayati baba wa taifa katika kitabu chake cha ‘Tujisahihishe’ cha mwaka 1962 mda mchache baada ya Tanzania kujipatia uhuru wake kutoka kwa waingereza na ningependa kunukuu;

“Tatizo kubwa la waafrika ni kuwa na majibu rahisi kwa matatizo makubwa”

Kwa mantiki ya mda uliopo na mambo yanavyoendeshwa kwasasa na baadhi ya viongozi wetu hatupaswi hata chembe kuhoji uwezo wa mwalimu nyerere katika kuchambua mambo na kueleza bayana hulka na mienendo ya watendaji ambao wamepewa dhamana ya kuliongoza taifa na kulivusha katika bahari ya umaskini ambao hadi sasa tiba yake imebaki kuwa ndoto za alinacha.

Katika nchi yetu ambayo wananchi wake wamekuwa wakiishi kwa matumani ya kuboreshewa maisha yao hali ya kukata tamaa inazindi kuongezeka hasa wanapopata fursa ya kusikiliza majibu ya kero zao kutoka kwa viongozi wao ambao waliwapa nafasi ya kuwaongoza. Majibu ya kisera au kimkakati kutoka kwa viongozi hao mara nyingi yamekua hayakidhi haja na kiu ya wananchi katika kuwaondelea matatizo yao.

Viongozi wetu wamekua wanaongozwa na mazoea ya ‘Funika kombe,mwanaharamu apite’ katika kero na matatizo makubwa ya kiuchumi,kijamii na kisiasa yanayowakabili wananchi wao na kuacha mizizi ya matatizo hayo ikiendelea kujichimbia katika maisha yao bila ya hata kuwa na uhakika wa kuiona kesho au kutambua hatma yao.

Ukiamua kufanya tathmini ya matatizo ambayo yamekuwa yakiendelea kuitatiza nchi yetu ijapokuwa ukiyatazama yapo ndani ya uwezo wetu ni wazi kuwa utakubaliana na hayati mwalimu nyerere katika hili la tabia ya viongozi wetu kutoyapatia majibu matatizo na kero zinaoendelea kudhoofisha nyonyo za wananchi wao ambao waliapa kwa vitabu vya mungu kuwa wangewatumikia kwa moyo na nguvu zao zote.

Ni aibu kwa nchi yetu kuendelea kushuhudia migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambayo imefikia hatua ya kugharimu maisha na mali za watanzania wenzetu. Tumekuwa tukiamini matatizo kama hayo yangetokea katika nchi ambazo zina uhaba wa rasilimali kama ardhi na maji lakini siyo kwa nchi yetu ya Tanzania ambayo mwenyezi mungu ameibariki kwa namna ya kipekee katika hili. Majibu sahihi ya kisera na kimkakati ya matumizi sahihi ya rasilimali hizo ni wazi yamekosekana na kulifanya tatizo hili liendelee kuonekana kama ni donda ndugu.

Matatizo yanayotokana na sera ya ubinafsishaji wa rasilimali tatika sekta mbalimbali kama madini,viwanda au mashirika ya uma yameendelee kuliandama taifa letu kutokana na hulka hizo hizo za viongozi wetu kuendelea kutoka majibu katika masuala tete yanayohitaji umakini na busara katika utatuzi wake. Tatizo la mgodi wa north mara ulioendelea kutiririsha maji yenye kemikali za sumu na kuathiri maisha ya watu na viumbe hayakupaswa kutolewa maji ya kukatisha tamaa kwa kiwango kile eti ‘ mgodi ulianza uzalishaji kabla ya sheria ya mazingira haijantungwa’. Majibu kama haya kutolewa na viongozi waliopewa dhamana kubwa yanawakatisha tamaa wananchi wetu na kuwafanya wajihisi yatima katika nchi yao.

Ukijaribu kuangalia matatizo katika sekta ya elimu ambayo ni tegemeo na msingi katika ustawi na maendeleo ya taifa lolote lile utakuta sababu ni ile ile ya kutotoa majibu yanayokidhi haja ya tatizo lenyewe na kwa wakati muafaka. Matatizo ya maslahi walimu ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo katika sekta husika yamekuwa yakipewa majibu rahisi bila kuwepo kwa mikakati endelevu ya kuyatatua na hali imeendelea kuwa hivyo hivyo kwa matatizo ya mikopo na migomo ya mara kwa mara katika taasisi za elimu ya juu nchini.

Matatizo ya njaa na upungufu wa chakula wa kila mara yanayoendelea kuwakabili wananchi wetu yanatokana ni matokea ya kila mara ya viongozi waliopewa dhamana katika sekta husika kuendelea kubwabwaja siasa katika mambo ambayo kimsingi yanahitaji utekelezaji tu. Kauli mbiu zinazobuniwa kila mara na kyumiwa kama mtji wa kisiasa haziwezi kutuondoa katika matatizo hayo bali ni kuwa watu wa vitendo kwa kutekeleza yale yote ambayo tulishayaazmia huko nyumba.

Azimio la iringa la siasa ni kilimo lilipaswa kutiliwa mkazo na kuongezewa nguvu nguvu tu kwani lilishaainisha kila kitu lakini likabaki suala la utekelezaji tu kwaiyo hatuhitaji misamiati mipya katika suala la kuborsha kilimo na kukifanya kiwe chenye tija na hatimaye kuwaondolea wananchi wetu umaskini ambao umekuwa ukiwaandama tangu wapate uhuru.

Matatizo ya mda mrefu ya nishati ya umeme ambayo ni muhimu katika ukuaji wa sekta ya viwanda ambayo ingeweza kuchochea maendeleo katika sekta nyingine yamekuwa ni kama yanapuuzwa kwa viongozi waliopota kuongoza sekta hiyo. Imekuwa ni kawaida kwa kila waziri anayepata fursa ya kuongoza sekta hiyo kutoa ahadi na kupanga mikakati isiyotekelezeka na kuondoka bila kuacha matunda yoyote kwani wameonekana hawatambui au wanapuuzia kwa makusudi ile dhana inayojulikana kwa kizungu kama ‘forward and backward economic linkage’ ambayo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa lolote duniani.

Majibu ya kila mwaka ya mawaziri hao kama vile ‘Serikali imejipanga kutumia vyanzo vingine kama makaa ya mawe, upepo na mwanga wa jua katika kutatua tatizo la umeme nchini’ hayatalisaidia taifa hili kuondokana na tatizo hilo kama hakutakuwa na dhamira za dhati kushughulikia uozo uliopo katika mikataba mbalimbali ya uzalishaji umeme ambayo imekuwa haina tija kwa taifa letu.

Matatizo ya ufisadi yanayoendelea kuikumba nchi yetu ni matokea ya uundwaji sheria na kanuni ambazo zimekuwa hazina meno ya kuyakabili. Majibu ya ‘Mheshimiwa spika,uchunguzi bado unaendelea’ yanazidi kulitumbukiza taifa hili katika hatari kubwa ya kuwafanya watumishi waendelee kujikita katika mambo ya kifisadi yasiyokuwa na manufaa kwa taifa letu. Katika akili ya kawaida ukijiuliza ni kwanini wale waliofikisha nchi yetu katika mikataba mibovu kama ya Richmond hawajachukuliwa hatua hadi sasa majibu yake ni wazi kuwa hayakidhi haja.

Hakika mambo haya yanakatisha tamaa na hata kuchafua dhamira na juhudi za viongozi wengine serikalini katika kuwaletea wananchi maendeleo. Ni jambo la kukatisha tamaa kwani imekuwa ni kawaida kwa matatizo ya kisekta ambayo yako ndani ya uwezo wa watu waliopewa dhamana ya kuongoza sekta hizo kusubiri hadi viongozi wakuu wa serikali kama raisi au waziri mkuu kuyatolea tamko huku hao wakendelea kuuchapa usingizi na kubwabwaja maneno yaliyojaa kila aina ya hila na ubabaishaji. Tatizo la mapigano ya koo huko tarime au msongamano wa makontena katika bandari zetu halipaswa kusubiri hadi viongozi wakuu wan chi kama rais au waziri mkuu walitolee tamko.

Bunge kama chombo chenye wajibu wa kuishauri na kuisimamia serikali katika majukumu yake linapaswa kujitakasa upya na kuanza kutekeleza wajibu wao wa msingi. Mheshimiwa spika Samwel sita ambaye anapenda kutambulika kama mzee wa ‘KASI NA VIWANGO’ anapaswa kuitekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati alipochaguliwa kuliongoza bunge ya kutovumilia majibu rahisi ya mawaziri katika mambo yenye maslahi ya kitaifa.

Mungu ibariki Tanzania yetu na viongozi wetu.

1 comment:

imanauliya said...

Nice blog and article, thanks for sharing. However want to statement on few common issues, The website taste is great, the articles is in point of fact excellent
Vimax asli
Vimax pills
Obat perangsang wanita
Boneka Full Body
Obat Vimax
Meizitang Botanical
Obat Pelangsing Alami
Celana Hernia