HATMA YA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA NA UVAAJI WA SARE ZA KISIASA SEHEMU ZA KAZI ZANZIBAR.
Mojawapo ya mambo ya msingi katika utoaji wa huduma za kijamii ni kutobagua watu katika misingi ya kidini,itikadi za kisiasa na makabila.Siasa za Zanzibar kama mjuavyo ziko tofauti sana na sehemu nyingine za Tanzania kwani kila kitu kimekua kikipewa tafsiri nyeti ya kisiasa hata kama kikiwa chema kiasi gani.
Nilishawahi kuandika katika gazeti tando hili juu ya uhasama uliokuwepo kati ya watu wa pande mbili hizi za Unguja na Pemba katika masuala mbalimbali ya kijamii kama vile kuzikana na hata katika biashara.Watu walikua wakisusia kuzika wafu kwasababu tu huyo ni MUUNGUJA au MPEMBA!au kununua bidhaa sokoni kutoka kwa mtu ambaye anatoka pande nyingine ya kisiwa hiki.
Kwa watu ambao wako nje ya kisiwa hiki wanaweza kudhani hali sasa ni shwari tangu uchaguzi mkuu ulipomalizika mwaka jana,La hasha! kwani bado watu wako katika sherehe za ushindi na maombolezo ya kushindwa katika kinyang’anyiro kilichopita.Huku tukiwa bado tunasubiri kwa hofu nini matokeo ya kauli ya katibu mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha CUF aliyoitoa juu ya mustakabali wa hali ya kisiasa Zanzibar ambayo alitamka wazi kua iko mikononi mwa viongozi wakuu wa tano(5) wa chama hicho nimeona ni busara kulisemea lile ambalo kwa namna moja au nyingine linaonekana kuchochea uahasama wa makundi haya mawili.
Utumishi wa umma unaongozwa na maadili katika utoaji huduma kwa wanajamii kama nilivyosema hapo awali bila ubaguzi wa aina yoyote ile iwayo.Lakini ni jambo la kushtukiza na kutia wasiwasi pale unapoona watumishi muhimu wa umma wakiwa katika sare za vyama vyao vya kisiasa katika kazi ambazo hazihitaji ushabiki wa aina yoyote ile wa kisiasa.Hivi kama mtu alikua anaweza kukataa kumzika mwenzake eti kwasababu ya tofauti zao kisiasa,JE chuki hizo haziwezi kuendelezwa hata katika huduma za afya,elimu na nyinginezo???
Kuna umuhimu gani kwa mtu kuvaa kofia,shati,kanga na beji ya chma chake wakati akijua wazi haileti picha nzuri kwa watu wa upande mwingine.Ushabiki kama huu unaoibua na kuchochea jazba za kisiasa kwanini ziendelezwe huku tukijua wazi hazina muelekeo au mwisho mzuri????Nilishawahi kusikia naibu waziri kiongozi akikemea tabia hiyo wakati wa ziara yake aligusia jambo hilo lakini nadhani ushabiki wa kisiasa walionao viongozi unakwamisha utekelezaji wake.
Haya ni masuala ambayo yakiangaliwa kwa juu juu yanaweza yasionekana kua na madhara,lakini kwa kuzingatia historia ya uhasama wa kisiasa inayoendelea kujikita katika kisiwa hichi,basi ni wazi kua hayo si masuala ya kufumbia macho hata kidogo na ni vyema viongozi husika kuchukua hatua zinazostahili kukomesha hali hii.
3 comments:
Materu habari hii imenichoma sana na nimetumia baadhi ya hoja zangu katika makala ya nyumbani maana naona suala la Takrima linaweza kupata majibu na pia makala yangu ya Mkapa kutaja mali naona imeulizwa Bungeni kuhusu watumishi wa umma kutaja mali pia wanapoacha ofisi sijui lakini taratibu tutafika ila inaumiza sana.
Nilidhani beji, fulana, kofia, n.k. zenye nembo au rangi za vyama huvaliwa wakati wa kampeni tu, kisha vinawekwa sandukuni.
Kama ulivyosema Materu, ,mambo mengine huonekana kama mzaha vile hadi inapokuwa kweli.
Ndiyo hali halisi, watanzania tumeshindwa kutofautisha serikali na chama, au, utanzania na u-ccm, cuf, tlp, chadema na wengine.
Utakuwa siku ya sherehe za uhuru wanakuja watu wamevalia sare za ccm na kuimba nyimbo za ccm. huwa sielewi kitu hiki, kama ni chama kilicholeta uhuru sio ccm ni Tanu au afroshiraz party, wangekuwa wanavaa sare za vyama hivi ningejitahidi kuwaelewa lakini sio wanavyofanya.
Nchi inagawanyika kwa kasi sana ingawa hatuni, kama hakuna sehemu ambako tunakaa pamoja na kujumuika bila kuonyesha tofauti zetu basi tunajimaliza wenyewe.
Naona siku sherehe za uhuru zikienda mbeya wanyakyusa, ambao siku hiyo watakuwa wengi, wataigeuza hiyo siku iwe ya kinyakyusa! tujiangalie tena.
Post a Comment