Tuesday, March 30, 2010

HEKIMA: KARAMA ILIYOTOWEKA KATIKA MAAMUZI YA VIONGOZI NA WATENDAJI SERIKALINI

Historia ina nafasi kubwa sana katika kuendeleza ustaarabu na imani kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.Matendo makuu ya kihistoria yaliyofanyika ktika kiwango cha juu cha busara na kwa kufuata maadili ya kazi na wakati husika nayo huwa ni chachu katika kudumisha na kuimarisha dhana ya utawala bora katika jamii husika.

Vizazi vilivyopo na vijavyo vinatakiwa kujifunza yale mema ambayo viongozi au watawala wao waliyasimamia na kuwaletea maendeleo.Hii ndio kazi ya historia chanya inayolenga katika kuimarisha nidhamu na imani kwa vizazi vilivyopo na kuchocchea hamu ya kujifunza au kuongeza bidii katika utendaji katika muelekeo au nia ya utendaji bora wa kuvuka viwango au kuweka rekodi.

Histoiria imekua ikituambia kuwa,nchi zilizoendelea kama ulaya magharabi na marekani na zinazoendelea kwa kasi kubwa kubwa kama Korea kusini,taiwani,Singapore zilifika huko kwa mchango mkubwa wa viongozi wao waliotambua umuhimu wa kuweka maslah ya taifa mbele katika kuletea jamii zao ustawi unaostahili.

Dhana ya uwajibikaji unaozingatia maadili ya utendaji kazi huwa ni chachu kubwa katika kunoa fikra za watendaji wetu na kushadihisha umuhimu wa kutumia hekima na busara katika utendaji kazi na maamuzi yanayohusu maisha ya wananchi na kutoa muongozo juu ya mustakabali ya nchi husika katika kujiletea maendeleo na kukuza ustawi wa jamii yenyewe.

Maendeleo ni hatua inayoratibiwa kwa kuzingatia vipaumbele ambayo jamii yenyewe imejiwekea katika kuwatumikia wananchi wake.katika mchakato huu viongozi au watendaji ni wadau wakubwa wenye dhamana ya kutoa muelekeo au muongozo wa mambo yapi yafanyike ambayo yataleta tija na ufanisi kwa jamii wanayoihudumia.

Utangulizi huu unatufanya sisi kuanza kutafakari kwa kina maamuzi mbalimbali yanayofanywa na viongozi wa kisiasa au watendaji serikalini katika kutimiza wajibu wao mkubwa wa kuwaletea maendeleo wananchi.

Tangu miaka ya katikati ya themanini hadi sasa,serikali yetu imekua katika kasi ya ajabu kuetekeleza maboresho mbalibali ya kisera katika sekta za kijamii na kiuchumi ambayo kwa pamoja wananchi wamekuwa wakielezwa kuwa yana lengo la kuboresha maisha yao na kuwaletea maendeleo.Viongozi hawa kimsingi wamekuwa wakiaminiwa katika kiwango kikubwa.
Mkataba kati ya watawala na watawaliwa unaofahamika kama social “contract” umekua ukitoa fursa kwa vingozi na watendaji wetu hawa kutekeleza majukumu makubwa kwa niaba yetu wananchi tukiwa na imani kuwa maslahi ya walio wengi yanazingatiwa.Maswali ya kuuliza katika namna maamuzi haya yanafanyika ni mengi na ambayo mara nyingi yamekua yakikosa majibu thabiti na ya kuridhisha kutoka kwa wale waliopewa dhamana.

Ubinafishaji wa mali za uma na rasilimali za kitaifa ni sera mbayo imekuwa ikipewa msukumo mkumo katika serikali ya awamu ya tatu na yeyote aliyeonekana kupinga sera hiyo amekua akionekana kama adui mkubwa wa maendeleo na anayepaswa kuhukumiwa kwa kesi ya kuhujumu harakati za kitaifa za ukombozi wa kiuchumi.

Wananchi wengi kwasas hawaonekani kuogopa kuhoji maamuzi ya watendai na viongozi wao.Wananchi wanazidi kutambua kuwa wana mchango na jukumu kubwa katika kuratibu na kusimamia mambo yenye muelekeo wa kukomboa mustakabali wa taifa lao.Wananchi wengi wameanza kupinga sera ya ubinafsishaji ambao kimsingi imekua ikitekelezwa kwa ubabaishaji wa hali ya juu na kuendelea kugharimu maisha ya wananchi wazawa.

Vijana ambao wako wengi nao wanazidi kusimama imara bila woga na kutoa wasiwasi wao juu ya hekima zinazowaongoza viongozi wao katika kufikia maamuzi mbali yanayohusu maisha yao katika nchi yao ambayo wanazidi kutambua kuwa nao ni wadau muhimu na sio watawala au viongozi waliopewa jukumu la kuwaongoza.

Ukiona wanajamii wananza kuhoji uwezo wa kufikiri wa viongozi wao basi ujue kua mambo si shwari tena na jitihada zinapaswa kufanyika kuondoa hatari hii ya kupoteza imani kwa viongozi na watendaji ambao wana jukumu la kufanya maamuzi na kusimamia maamuzi hayo kwa manufaa ya wanajamii wanaowaongoza.
Ukitembea katika maskani za vijana na barabarani utasikia wananchi wanahoji,Hivi hawa viongozi wetu wanatumia akili kufikiri?Hivi maamuzi wanayosimamia yanatambua kuwa kesho ipo? Hivi vizazi vijavyo vijifunze yapi mema kutoka kwao?Ni upi urithi wa fikra wanaowaachia vizazi vilivyopo na vijavyo?Je,na sisi tuige ubabaishaji kama wao katika mamuzi?

Maswali kama hayo yamekua yanaulizwa bila majibu ya kutia moyo na kuwaacha watu na hasira ambazo ni wazi zinawakatisha tamaa.Katika maongezi yao kuna baadhi wanapendekeza vijazi vijavyo vifukue makaburi ya voingozi wao waliowatangulia na kuanza uchunguzi wa kupata uhakika wa uwezo wao wa kufikiri na kiwango cha busara kilichokuwa kinawaongoza kufikia maamuzi.Hapa namkumbuka mwanasayansi mmoja wa kimarekani aliyetoa matokea ya utafiti kuhusu uwezo wa akili kati ya watu weusi na weupe.Vijana wetu wanasema utafiti huo ulikua unawalenga viongozi wa na watendaji wa serikali za kiafrika hususani Tanzania.

Sera ya ubinafsishaji inayopigiwa chapuo na benki ya dunia na shirika la kimataifa la fedha imethibitika kuwa haina tija katika kuwaletea wananchi wetu maisha bora na badala yake imeonekana ni kama msumari wa mwisho unaopigiliwa katika makaburi ya nchi maskini duniani na zile zinazoendelea ikiwemo Tanzania ambayo maamuzi mengi ya viongozi wake yameigharimu na kuendelea kugharimu ustawi wa wananchi wake.

Katika yote hayo hekima inaonekana kukosekana katika kila mambo au maamuzi mengi yanayofanywa na viongozi wetu.Vizazi vijavyo ni kama vitabaki bila mwalimu wa kujifunza kutoka kwao na kuendelea kuweweseka na kujikuta wakitumbukia katika shimo la taka lilikosa staha ya kuchammbua zuri na baya la kuhifadhi.

Viongozi wetu wamekuwa wakihudhuria warsha za kimataifa za kimkakati kila kukicha lakini matunda yake yamekua ni kama ndoto.Viongozi wamekua wanashiriki kikamilifu katika maandalizi ya sera na mikakati ya kiutekelezaji ya kibabaishaji lakini baadae wamekua wakiikana na kuonea aibu kuwa sehemu ya hiyo mikakati baada ya licha ya kutambua kila awali kuwa haina tija.
Wananchi wanakosa subira ya kuhoji iwapo viongozi wao wanatumia vilevi kabla ya kushiriki katika michakato mbalimbali ya upangaji sera na kufanya maamuzi yenye malengo ya kuinua maisha ya watu wake.Mifano katika hili ni mingi sana naya kukatisha tamaa.Kuna msemo wa siku nyingi unaosema kuwa ‘Ukibebwa na wewe ubebeke au ujishikile’.Msemo huu pia amekea akiutumia rais kikwete katika baadahi ya hotuba zake kwa wananchi.

Nchi wahisani wamekua wakijitahidi kutoa misaada mbalimbali za kimaendeleo tangu uhuru kwa nia moja kubwa ya kuboresha maisha ya wananchi wetu.Matokeo ya miradi ambayo imekua ikifadhiliwa na wenzetu hawa ni kama hayapo.Ukifika wilaya ya mbarali utasikia hadithi za kusikitisha katika ule mradi wa umwagiliaji uliofadhiliwa na serikali ya wachina kama zawadi chini ya utawala wa Mao Tse tung mikana ya sitini.

Mfereji huo mkubwa na wa kisasa uliokua matumaini kwa wananchi wa eneo husika sasa unabaki kuwa ndoto na chanzo cha manungu’niko kwa wakazi wa eneo hilo.Serikali mara zote imekua ikitoa kisingizio cha kukosa fedha za uendeshaji miradi na kufikia maamuzi ya kubinfsiha.Mradi huu wa umwagiliaji ulikua unastahili usimamizi na sio mtaji kama wengi wanavyopsawa kuamini.Katika mazingira haya ndo yanayowapelekea wananchi kuhoji busara na hekima inayowaongoza viongozi wao katika kufikia uamuzi wa kubinafsisha mradi kama huu wa umwagiliaji.

Ni wazi kuwa viongozi hawa wanatambua kuwa asilimia kubwa ya wakazi wa eneo hili huetegemea kililmo cha mpunga katika kuendesha maisha yao.Kubinafsisha mfereji huo kwa mtu binafsi ni kuwasaliti wananchi ambao kimsingi wanapaswa kunufaika nao.Hivi sasa aliyekabidhiwa mashamba hayo na mfereji huo mkubwa uliofadhiliwa na serikali ya watu wa china anawakodoshia wazawa.Hakika huu ni unyonyaji ulio dhahiri kwa wananchi.

Ni hekima gani iliyoyumika kuubinafsisha mradi huu kwa mtu mmohja na kuwaacha maelfu ya wananchi wa maeneo hayo watumwa na wasio matumaini katika kuboresha maisha yao wakitegemea kilimo ambacho ni wazi kuwa ndio mkombozi wa wakazi wa eneo hilo?Ni wazi kuwa viongozi kwasasa wanatambua madudu katika utekelezaji wa maamuzi hayo,lakini suala kubwa lililobaki ni,nani amfunge paka kengele katika kubadili maamuzi hayo dhalimu kwa wananchi wa maeneo hayo.

Rasilimali mbalimbali za kitaifa zimekua zikipotea kutokana na maamuzi mbalimbali ya viongozi wetu yanayoweka hekima kando kwa ajili ya maslahi binafsi.Vizazi vyetu vijufunze yapi mema katika yote haya ya kibabaishaji yanayoendelea kufanywa na viongozi.Kubinafisha misitu,migodi kwa mikataba isiyo na kikomo au ya kibabashaji,je ilihusisha hekima gani katika kufikia huko?Hizi ni changamoto ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na viongozi wetu badala ya kuzifanya za kiitikadi ili kuweka mazingira kwa vizazi vilivyopo na vijavyo kurithi mema kwa maslahi ya taifa letu.

No comments: