Tuesday, March 30, 2010

MCHAWI WA MAENDELEO YA AFRIKA NI WAAFRIKA WENYEWE

Bara la Afrika linaendelea kupita katika wakati mgumu kwa miongo kadhaaa sasa. Wananchi wake wanashindwa kujua ni lini ndoto zao za kuishi maisha bora baada ya kuteseka kwa kipindi kirefu zitakuwa kweli. Kila kukicha wananchi wanaendelea kukata tamaa na kubaki wakiitamani jana kuliko leo na kesho kwani mambo yanazidi kwenda mrama na hakuna dalili ya muujiza kutokea utakaowafanya wao wajihisi ni sehemu ya dunia ya sasa inayafaidi matunda ya sayansi na teknolojia katika karne hii ya ishirini na moja.

Kumekuwa na mijadala mbalilmabi inayoendelea katika kile kinachoonekana kumtafuta mchawi wa matatizo yanayoendelea kulitafuna bara letu hili kwa mda mrefu ambayo imeibua mitizamo tofauti. Kwa upande wa Afrika, historia imeendelea kutumiwa na viongozi wetu kama chanzo cha matatizo hususani ya umaskini yanayoendelea kulikabili bara letu na wananchi wake licha ya miongo kadhaa kupita tangu nchi hizi zijipatie uhuru wake kutoka kwa wakoloni.

Ni kweli kwamba ukoloni na biashara ya watumwa ulichangia kwa kiasi fulani kudumaza maendeleo ya bara letu la Afrika lakini hakuna mantiki ya kuendelea kuwa watumwa wa historia na kujifunga katika fikra ambazo kimsingi hazina mashiko kwasasa kwani ni kipindi kirefu kimepita kwa sisi kuweza kukaa na kujipangia dira ambazo tunaamini zingetupeleka kule tunapotaka kufika.

Wakati viongozi wetu wa bara hili wakiendelea kutafuta visingizio na kupiga ramli kumtafuta mchawi anayekwamisha ustawi wa maendeleo ya wananchi wao na nchi zao wanakumbushwa ukweli mmoja ambao wengi wao wamekuwa wakiendelea kuukwepa kuujadili kwa uwazi kwa kipindi kirefu sasa na kubakia kubwabwaja visingizio ambavyo kimsingi havilengi kuujua ukweli wa mambo bali kujijengea uhalali kwa wananchi wao kwamba matatizo ya nchi zao hayatokani na wao kutowajibika ipasavyo.

Akihutubia bunge la jamuhuri ya watu wa Ghana Julai 11 2009 wakati wa ziara yake ya pili katika bara la Afrika baada ya ile ya Cairo,rais Barrack Obama wa marekani ambaye ana asili ya Afrika aliamua kuwapsulia ukweli viongozi hao wa afrika ambao kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa wakishindwa kuukabili ukweli huo kwa uwazi unaostahili. Raisi Obama aliliambia bunge la Ghana na napenda kutoa tafsiri isiyo rasmi “Kitu kinachokwamisha maendeleo ya Afrika ni tabia ya viongozi kuendelea kutoukubali ukweli kuwa utawala mbovu na rushwa ni sababu kuu katika hilo”

Ni ukweli ulio wazi kuwa dhana ya utawala bora imeendelea kupewa tafsiri finyu na kufananishwa kama utamaduni wa kimagharibu ambao hauna nafasi katika mazingira yetu ya kiafrika. Watawala wetu wameendelea kudhani kuwa,kwa kufanya changuzi katika nchi zao ni kielelezo mahsusi cha wao kutekeleza dhana hiyo kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kimeendelea kuwapa ujasiri wa kujitangaza mbele za jumuiya za kimataifa kuwa wanatekelezo kwa vitendo dhana hiyo.

Ukijaribu kuoanisha hoja hizo na hali inavyokwenda hupati shida ya kutambua ni kwanini watawala wa bara hili wanapata shida ya kutambua dawa za matatizo yanayozikabili nchi zao kwa kipindi kirefu sasa na raisi kikwete anaweza kuwa mfano mahsusi katika hilo. Wakati alipohojiwa na chombo kimoja cha habari cha magharibi alisema hata yeye hajui kwanini bara letu la Afrika na hususani nchi yetu vimeendelea kulowea katika dimbwi la umaskini licha ya kuwa na kila rasilimali zinazohitajika katika kuwaletea wananchi wetu maendeleo kwa kasi.

Tunatambua kuwa njia pekee ya kuliondoa tatizo ni kukubali kulikabili tatizo lenyewe na siyo kujifanya kuwa wewe au mimi siyo sehemu ya tatizo lenyewe. Dhana ya utawala bora ni pana na haipaswi hata kidogo kurahisishwa na kuonekana kama inaishia katika uratibu wa chaguzi mbalimbali ambazo kimsingi pia zimekuwa hazifuati misingi ya kidemokraisa.Hii ni tafsiri finyu ambayo kama haitapata nafasi ya kujadiliwa kwa upana itaendelea kutoa uhalali kwa viongozi wasiofaa kuendelea kukalia viti bila uwezo wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kama alivyogusia raisi Obama,bara letu na viongozi wake kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa wakiyatupia kisogo mambo muhimu kama utawala wa sheria na unaoheshimu haki za binadamu, uadilifu na uwajibikaji wa viongozi, uwazi katika uongozi au uendeshaji wa serikali, ushirikishwaji mpana wa wadau katika kufanya maamuzi ambavyo kwa pamoja vinakamilsha dhana nzima ya utawala bora.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa misingi hiyo licha ya kuwa ni ajenda ya siku nyingi inayopiganiwa na mataifa yanayoendelea na wanaharakati wa kimaendleeo imekuwa ikiukwa kwa kiwango kikubwa katika nchi zetu za kiafrika na viongozi wetu ndo wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa haipati nafasi ya kumea katika bara hili kwani inapinga moja kwa moja tabia na hulka za viongozi hao katika stahili za uoendeshaji nchi zao.

Ni kweli isiyopingika kabisa kuwa maendeleo yetu yanategemea utawala bora kiambatano ambacho kinakosekana katika nchi zetu nying za kiafrika na kwa mda mrefu mno. Mifano kadhaa aliyoitoa raisi Obama inapaswa kuwafungua macho viongozi wetu na kuanza kuyafanyia kazi maeneo yale ambayo yamekuwa yakikwamisha maendelo ya nchi zao na wananchi wao kwa ujumla.

Historia inatuambia kuwa nchi za mashariki ya mbali katika bara la Asia ambazo katika miaka ya sitini zilikuwa katika kiwango sawa cha maendeleo na nchi zetu za afrika na pengine baadhi ya nchi zetu kuzipita leo hii imebaki kuwa historia kwani zimefanikiwa kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika kila Nyanja na kuziacha nchi zetu zikiendelea kulowea katika umaskini.

Raisi Obama alitolea mfano wa kusikitisha kwa nchi zetu za Afrika kama Kenya na nyinginezo ambazo zilikuwa na uchumi mkubwa kwa mtu mmoja mmoja kuliko korea kusini, Singapre, Taiwani lakini kwasasa zimepitwa vibaya. Ni kweli iliyo wazi kuwa nchi hizi hazikutumia uchawi kufika huko waliko bali ni kujipanga kiuongozi na kuweka vipaumbele vyao sawa na kwankutumia vizuri rasilimali chache walizonzao kwa manufaa ya nchi yao na wananchi wao kwa ujumla.

Matumizi mabaya ya rasilimali yamekuwa yakiendelea kukwamisha juhudi za nchi zote kujikwamua pale zilipo kwani kiasi kikubwa kimekuwa kikitumiwa katika kuimarisha dola na vyombo vyake vya usalama ili waendelea kujinufaisha wao wenyewe na kuwaacha wananchi wao wakiendelea kubaki bila mtetezi.

Ghana na Botswana zinachukuliwa kama mfano wa uwezekano wa bara hili kuendelea ikiwa tu watawala au wanasiasa waacha uzandiki katika nafsi na dhamira zao kuongoza kwa kutumia rasilimali zao walizonazo kama madini na mafuta katika kuwaletea wananchi wake maendeleo ya haraka.

Mustakhabali wa afrika uko juu ya sisi wa waafrika wenyewe ikiwa tutaamua kuyakabili matatizo yetu kwa nguvu mpya, ari mpya na kasi mpya itakayojitafsiri zaid katika matendo na sio hadaa ya kujipatia kura na kujiejengea uhalali wa kushika hatamu ya kuendelea kutafuna rasilimali za nchi kwa manufaa binafsi.

Hakuna sababu au uhalali wowote kwa magonjwa na migogoro viendelee kuvuruga maeneo mengi ya bara letu na kusababisha wananchi wetu wapoteze maisha kwa mambo ambayo viongozi wetu wameendelea kuyakumbatia. Ile dhamira ya utumishi inayopaswa kuwa msingi wa kufanya kazi kwa maslahi ya uma inapaswa ihuishwe kwa kuweka taasisi huru zinazoweza kuchochea uwajibikaji wa wale wote wanaopewa dhamana za kiuongozi.

Hakuna mtu anayetaka kuishi katika jumuiya ambapo utawala wa kisheria unageuzwa kuwa utwaala wa kikatili na hongo unaolenga katika kuwanyima wananchi wake haki za kimsingi zinazolenga katika kuwaboreshea maisha yao. Wananchi ambao kimsingi ndio nguvu kazi tegemewa ya kuziletea nchi zao maendeleo zinapaswa kuheshimiwa na kupewa fursa stahili kama sehemu muhimu ya jamii katika kuleta mageuzi kwenye nchi zetu kwa kushiriki kikamilifu katika harakati hizo.

Tunategemea nini iwapo mabunge yetu ambayo yanategemewa kuwa taasisi muhimu za kusimamia utendaji wa serikali zetu na viongozi wake yamegeuka kuwa jukwaaa la ushabiki wa kisiasa unaojikita zaidi katika kutetea na kufunika maovu ya watawala kuliko kutetea maslahi ya umma inaouwakilisha? Hulka za taasisi hizi hazileti matumaini yoyote kwa wananchi zaidi ya kuendelea kuwajengea hali ya kujiamini na kiburi watawala na serikali zao katika harakati zao za kuendelea kutafuna rasilimali za uma.

Hata misaada ya dola bilioni tatu ambazo serikali ya marekani imeahidi kuzitoa kwa kile ilichokiita kuchochea kilimo cha uzalishaji chakula kwa bara la Afrika ni wazi zitakuwa hazina tija au matokeo yoyote kama dhana nzima ya utawala bora haitapewa kipaumbele katika taasisi za kiutawala kwenye nchi zetu hizi ambazo zimeendelea kujijengea mazingira ya kuwa ombaomba kwa kipindi kirefu sasa. Zabuni katika ujenzi wa miundo mbinu ya barabara huishia mikonini mwa wajanja wachache na kuacha sekta husika zikiwa hoi kabisa.

Tunategemea nini ikiwa misaada yenye thamani ya mamilioni za dola za kimarekani zinazolenga kusadia matatizo ya kiafya kama ukimwi na kifua kikuu zanaendela kuishia kwenye matumbo ya watu wachache na kuwaacha maelfu ya wananchi wao ambao ndio nguvu kazi pekee ya kujiletea maedeleo wakiendelea kupoteza maisha kwa kukosa dawa?

Tunategemea nini ikiwa rasilimali za taifa kama madini,mafuta na mazo ya misitu yakiendelea kusafirishwa nje ya nchi kwa kushirikiana na taasisi zetu za forodha ambazo zinakosa misingi ya maadili ya utawala bora na kuzifanya nchi zetu ziendelee kuwa tegemezi? Ni kwanini vyombo hivi visimulikwe na kuwawajibisha wale watendaji wote wabovu ambao wanaongozwa na misingi ya ubinafsi kuliko ile ya maslahi ya uma.

Tunategemea nini ikiwa watu wanapewa nafasi za uongozi au utumishi kwa upendeleo na kuwaacha wenye sifa nje ya mfumo wa uendeshaji utakoasadia kuleta tija na changamoto makini katika utendaji kazi unaolenga kuwaondolea wananchi kero na hatimaye kufufua maendeleo ya nchi zetu? Tusitegemea miujiza katika maendeleo ikiwa maeneo muhimu ya kimkakati wa kisera vitaendelea kuangukia mikononi mwa watu ambao kimsingi hawana sifa au uwezo wa kuyaongoza kwa ufanisi unaotakiwa.

Haya ni baadhi ya maeneo ambayo viongozi wetu wa kiafrika hawana budi kuyatazama kwa na namna ya kipekee na kuanza kuyafanyia kazi kuliko kuamua uendelea “Kuwa sikio la kufa ambalo kamwe halisikii dawa” kwa kushindwa kutambua chanzo au sababu ya matatizo yetu na kuendelea kutafuta mchawi kwa makosa yao wenyewe.

Mungu ibariki Afrika yetu na viongozi wetu.

No comments: