Tuesday, March 30, 2010

MITIZAMO YA AKINA IBIN BATUTA NA HULKA ZA WANASIASA WA TANZANIA YA LEO

Nchi yetu ya Tanzania tuipendayo kwa moyo wetu wote inapita katika wakati mgumu sana kisiasa na kiuchumi. Hakika ni kipindi ambacho historia itapata mengi ya kuandika kwa ajili ya vizazi vyetu vijavyo ambayo ni mategemeo ya walio wengi kuwa nchi yao itakuwa imeandaliwa vyema na kuwa sehemu salama ya kuishi huku kukiwa na misingi imara ya kuboresha maisha yatakayowawezesha kufurahia matunda ya uhuru ambao babu na bibi zao walijitoa mhanga kuyapigania.

Mtikiso wa kiuchumi unaoikumba dunia kwasasa na mawimbi ya demokrasia ambayo yameanza kuvuma kwa kasi kubwa katika nchi yetu na taasisi zake vinatupa fursa ya sisi kutafakari na kutoa mawazo yetu juu ya nini kifanywe haswa na wale watu waliopewa dhamana za uongozi katika serikali ili waweze kutekeleza wajibu wao na kutupitisha salama katika kipindi hiki kigumu na cha mpito ambacho kinahitaji hekima na uadlifu kwa kiwango kikubwa kuinusuru nchi au kizazi chochote.

Nchi yoyote ile au vizazi vyovyote katika ulimwengu huu ambao wamekua kwa namna moja au nyingine wakiidharau historia hujikuta katika wakati mgumu sana katika harakati zao za kujiletea maendeleo na hali huwa hivyo pia kwa binadamu ambao wamekuwa wakidharau maadili ya msingi ya vizazi vyao. Mila na utamaduni wetu wa kiafrika au kitanzania umekuwa ukituaminisha kwa namna ya kipekee kuwa wazee ni watu walio na busara ambao wosia au miongozo yao ni muhimu katika maendeleo yetu na kama tukifanya vinginevyo au kinyume na miongozo au mitazamo yao basi tutegemee madhara makubwa.

Nchi yetu na bara letu la Africa katika miaka ya mwanzoni mwa sitini na mwishoni mwa themanini zilipata bahati kubwa ya kuongozwa na watu wenye dhamira safi na kiu kubwa ya kuwaletea watu wake maendeleo yanayozingatia haki na usawa na yenye kukidhi haja au matakwa ya wananchi wetu. Ni viongozi ambao walikua na uadilifu mkubwa huku wakitanguliza hofu ya mungu mbele wakiamini wamepewa majukumu hayo ya kiuongozi si kwasababu ni wao pekee wenye uwezo wa kuongoza bali ni wito uliojikita katika mitazamo ya UTUMISHI ULIOTUKA ambao haulengi wao kujipatia kitu bali kuwapitia wale wananchi wanaowaongoza vitu vitakavyowawezesha kuboresha maisha yao.

Viongozi hao ambao wengi wao tayari wameshatangulia mbele ya haki walikuwa wakitumia mda wao mwingi kutafiti,kuandika,kuasa, kuonya na kufundisha yale mambo ambayo waliamini yangesaidia kujenga vizazi ambayo vinafuata maadili katika harakati zao za kujiletea maendeleo baada ya miongo kadhaa ya kutawaliwa. Sio tu kujiletea maendeleo bali kujijengea mazingira ya kuruhusu uadilifu utawale katika fikra za vizazi hivyo huku upendo ukiwa nguzo kuu ya wale wote wanaopata nafasi za kushika hatamu za ungozi wa nchi au taasisi muhimu za kiutawala ambavyo kwa pamoja ni mihimili muhimu ya kuleta na kudumisha amani.

Hakika waafrika na watanzania tumejaliwa mambo mengi muhimu ambayo tungeyatumia vyema yangeweza kutuletea maendeleo ya haraka, ya uhakika na makubwa. Sitapenda kuzungumzia utajiri wa kirasilimali tuliojaliwa nao kwani wengi wameshaandika. Leo ningependa kukumbusha wasomaji wetu utajiri wa kifalsafa,kimaadili na miongozo ya waasisi wa bara letu na taifa letu la Tanzania ambavyo kimsingi tungeamua kuviheshimu na kuvitumia tungefanikiwa kuwa na dola za kiutawala zinazoheshimu utu wa watawaliwa na kujenga misingi imara ya uwajibikaji unaofuata maadili ya kiuongozi wenye kuleta tija na unaoheshimu demokrasia ya kweli.

Ukianza kutafakari kwanini kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa kimaadili ya kiuongozi kwa wale walio katika nafasi za uongozi wa umma katika viwango vya kutisha kwa nchi zetu unaweza kurejea utangulizi wangu hapo juu kuwa inatokana na vizazi na viongozi waliopo ama kupuuzia misingi ya mawazo na maadili ya kiuongozi yaliyosisitizwa na waasisi na wazee wetu waliopata kuongoza nchi yetu na bara letu kwa ujumla.

Historia inatuambia watanzania kuwa Ibini Batuta,aliyepata kuwa mtawala na mwanaharakati katika ufalme wa morocco aliwahi kutembelea Zanzibar katika karne ya kumi na nne(14th C) katika moja ya ziara zake ndefu za kusisitiza umuhimu wa uongozi bora uliojengeka katika misingi ya kujitolea ili kuwaletea wale tunaowaongoza maendeleo yenye tija na ningependa kunukuu kipande kidogo cha maneno yaliyopo katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa ziara yake visiwani huko ili yawe msingi wa mada hii ya leo nanukuu;

“Tutakapofariki dunia,msitutafute kwenye makaburi yaliyopakwa chokaa,
bali tutafuteni kwenye mioyo ya wale tuliowasaidia kuboresha maisha yao”

Hakika ni maneno mazito yanayopeleka ujumbe mahsusi kwa wale waliopewa dhamana za kiuongozi katika jamii na nchi zao kwa ujumla. Vizazi vilivyopo na vijavyo vinatakiwa kujifunza yale mema ambayo viongozi au watawala wao waliyasimamia ambayo waliamini kuwa yakifuatwa na kutekelezwa yanaweza kuwa nguzo muhimu za kuwaletea maendeleo.Hii ndio kazi ya historia chanya inayolenga katika kuimarisha nidhamu na imani kwa vizazi vilivyopo na kuchocchea hamu ya kujifunza au kuongeza bidii katika utendaji kazi ulio bora wa kuvuka viwango au kuweka rekodi safi za utumishi.

Nilishawahi kuandika makala katika gazeti niliyoipa kichwa cha habari “Hekima: karama iliyotoweka katika maamuzi ya viongozi na watendaji serikalini” . Nilikuwa najaribu kutazama maamuzi mbalimbali yanayofanywa na baadhi ya viongozi waliopewa dhamana za kiuongozi katika nchi yetu na kutoa angalizo la wao kubadilika kwani vuguvugu lililopo linaweza kuifikisha nchi mahali pabaya kwani wananchi wameshanza kuhoji kiwango cha maadili na uwezo wa kiakili wa viongozi wao katika kufikiri, kuamua na kutenda. Wanahoji iwapo viongozi wao wanatumia akili kufikiri na iwapo maamuzi wanayosimamia yanatambua kuwa kesho ipo? Wanahoji pia ni upi urithi wa fikra wanaowaachia vizazi vilivyopo na vijavyo?

Maswali kama hayo yamekua yanaulizwa bila kupatiwa majibu ya kutia moyo na kuwaacha watu na hasira ambazo zinaendelea kunyong’onyeza nafsi zao na kuendelea kuwakatisha tamaa.Katika maongezi yao kuna baadhi wanapendekeza vijazi vijavyo vifukue makaburi ya voingozi wao waliowatangulia na kuanza uchunguzi wa kupata uhakika wa uwezo wao wa kufikiri na kiwango cha busara kilichokuwa kinawaongoza kufikia maamuzi mbalimbali yaliyopaswa kuchukuwa muelekeo wa kutafuta mbinu za kutatua matatizo yao ili waweze anagalao kuwakumbuka kwa siku zijazo na kuacha historia itakayotukuka kwa vizazi vijavyo.

Huo unaweza kuwa msingi wa kile kilichomsukuma Ibini batuta kutoa maneno yale katika ardhi ya nchi yetu na kwa kuzingatia hulka za viongozi wetu kama mawaziri na wabunge ambao wengi wamekua wakikiuka wazi wazi na kwa makusudi misingi ya maadili ya utumishi hivyo kuleta changamoto kubwa kwetu kuwakumbusha na kuwasimamia hao waliopewa dhamana kuonyesha utumishi bora kwa yale waliyoahidi kutekeleza na kutuletea maendeleo ambayo yataacha alama isiyofutika katika mioyo yetu.

Tatizo kubwa linaloonekana kwa viongozi wetu ni ama tabia yao ya kutopenda kusoma au kupuuzia machapisho au hotuba za waasisi na wanafalsasa wetu walioandika mambo mengi mema na muhimu ambayo yanaweza kuwa ni dira muhimu katika uongozi wa uma. Ubinafsi unaonekana kuchukua nafasi kubwa katika utendaji kazi wa viongozi wa serikali zetu na hata kufikia hatua ya wao wenyewe kuanza kunyoosheana vidole na kutuhumiana na hata kuomba mungu awalaani baadhi yao.

Katika lugha rahisi viongozi wetu waliopewa dhamana ya kuongoza sekta muhimu kama za afya,elimu na kilimo na nyinginezo wanapaswa kutafakari kauli ya Ibini batuta na kujiuliza wananchi wao wataenda kuwatafuta wapi pindi watakapokua wamemaliza jukumu lao la kuongoza wizara hizo au pindi watakapokua wametangulia mbele ya haki. Ni muhimu kwa wao kuanza kutafakari juu ya kile wanachopaswa kuacha kama alama ya uongozi uliotukuka .

Kwa mfano, Je wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu watawakumbuka mawaziri waliopata kuongoza wizara hiyo kwa lipi?? Walimu wa shule za msingi na sekondari hasa za vijijini wawakumbuke voingozi wao wenye dhamana kwa lipi?. Mahakimu halikadhalika wanaofanya kazi katika mazingira magumu ya kujenga taifa linaloheshimu sheria na haki watawakumbuka viongozi wao kwa lipi.Polisi nao ambao wamekuwa wakijitoa mhanga kulinda mali na maisha ya raia na viongozi wao watawakumbuka hao wenye dhamana kwa jambo lipi?

Wananchi walio katika maeneo ambayo rasilimali kama madini na mbuga za wanyama wananufaika vipi na wamewekewa mazingira gani yanayoweza kuwahakikishia kuwa wanafaidi matunda ya rasilimali walizojaliwa na mwenyezi mungu. Rejea kipindi cha je tutafika kilichorushwa na chanel 10 siku ya alhamisi na ujiulize, Je wananchi walio katika maeneo ya migodi kama kule tarime wanaoendelea kuathirika na kemikali zinazozalishwa katika migodi hiyo wawakumbuke wabunge na mawaziri wao kwa mema yapi? Je wananchi wawakumbuke viongozi wao kwa mikataba mibovu waliyoingia isiyo na tija yoyote kwa taifa?

Swali la msingi ambalo viongozi wetu wanapaswa kujiuliza na kutafakari ni je watanzania wawakumbuke kwa ubabaishaji wao watakapokuwa wametoka katika dhamana za uongozi au wameaga dunia? Uongozi wa kinafiki hautalipeleka taifa hili kokote na ni vyema viongozi waliopo madarakani na wale wanaoomba ridhaa ya kuongoza nchi hapa nazungumzia vyama vya upinzani wakatambua hilo. Ukitizama bunge kwasasa unaweza kupatwa kichefuchefu kwa jinsi wawakilishi wetu wanavyojifanya wamechachamaa kuwatetea wananchi wao kumbe ni hadaa tu ili wajihakikishie nafasi za kurudi tena bungeni kipindi kijacho ili waendelee kijineemesha nafsi zao kwa vipindi vijavyo. Ningependa kumalizia kwa kuwauliza viongozi wetu “Je watakapofariki dunia,tuwatafute kwenye makaburi yaliyopakwa chokaa,au kwenye mioyo yetu itakayowakumbuka kwa kutusaidia kuboresha maisha yetu”
Mungu ibariki Tanzania yetu na viongozi wetu.

No comments: