Tuesday, March 30, 2010

RAISI KIKWETE USIWAVUMILIE VIONGOZI WASIOWAJIBIKA

Rais kikwete wakati anahutubia bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania manamo tarehe 30 december 2005 mara baada ya kuibuka mshindi wa nafasi ya urais katika uchaguzi wa tatu chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi alitoa hotuba ya kusisimua na kuhuisha matumaini ya watanzania ambao wengi wao tayari walikuwa wamekata tamaa juu ya mustakabali wa maisha yao katika nchi yao ambayo wengi wao wamejitoa kwa dhati ya moyo wao wote kuijenga.

Mambo makuu mawili ambayo mheshimiwa rais alitumia mda mwingi kuyafafanua na kuyasisitiza wakati wa hotuba yake ile ni kwanza kuilinda na kudumisha amani na usalama wa nchi ambavyo waasisi wa taifa hili walitumia mda na nguvu nyingi kuvipigania na jambo la pili lilikua kuboresha maisha ya watanzania ambao walionyesha imani kubwa kwake kwa kumchagua kwa kura nyingi kitu ambacho hata raisi Kikwete mwenyewe alikiri kuwa ni deni kwake.

Binafsi namuheshimu sana rais kikwete na kutambua dhamira yake kama raisi katika kuwaletea wananchi wake maendeleo. Napenda kusema pia nakiheshimu chama cha mapinduzi kwa kuzingatia historia yake na waasisi wake katika jitihada za kuliongoza taifa katika wakati mgumu na kuwatumikia wananchi wake ambao waliendelea kuonyesha imani kwacho kwa miongo kadhaa sasa. Nimeamua kulisema hilo mapema ili ili watu wasiendelee kujenga hoja mufilisi pale tunapoandika mambo ambayo wenye njaa ya fikra thabiti wamekuwa wakiendelea kutunyooshea vidole kuwa tuna chuki na watawala na chama tawala ambacho kimsingi kimetukuza hata sisi.

Rais Kikwete wakati wa hotuba yake ile aliliambia bunge kuwa ‘Urais wake hauna ubia na mtu’. Maneno yale ni kama alikuwa anawaambia wasaidizi wake kuwa hatawavumilia pindi watakapoonekana kwenda kinyume na misingi ya kiutumishi unaolenga kuwaletea a wananchi maendeleo, kuwaondolea kero zao na hatimaye kujenga taifa imara lenye mikakati thabiti ya kujiondolea umaskini na kulinda misingi ya haki za watu na utawala wa sheria.

Ni kweli iliyo wazi kuwa raisi kikwete binafsi hawezi kulivusha taifa hili katika bahari iliyojaa changamoto mbalimbali kama umaskini, rushwa,maradhi, ujinga, unyimwaji haki na kuporomoka kwa maadili ya jamii ambayo imepelekea kuibuka kwa vitendo vyenye kuashiria uvunjifu wa amani na utulivu wan chi yetu ambayo kwa kipindi kirefu imefanikiwa kijijengea heshima katika jumuia za kimataifa.

Kwa kuzingatia ukweli huo ni budi kwa raisi kuteua watu ambao anawaamini kuwa na uwezo wa kumsaidia katika kutekeleza majukumu aliyopewa na wananchi ambao kimsingi ndiyo waajiri wake wakuu na mwisho wa siku atawajibika kwao. Changamoto ya kuwapata watu hao ni kubwa lakini kwa kushirikisha vyombo vyake vya usalama tulitegemea kuwa inaweza kuwa rahisi na kuwapatia wananchi watu ambao wanaongozwa kwanza na maadili ya utumishi uliotukuka ambao umejikita katika misingi ya maadili ya utoaji huduma.

Ukiwa mfuatiliaji wa mambo yanavyokwenda katika nchi yetu lazima utawaonea sana huruma viongozi wakuu wa nchi kama raisi, waziri mkuu au makamu wa raisi wanavyohangaika huku na kule katika kutatua kero ambazo kimsingi wasaidizi wao kama mawaziri,wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wangepaswa kuzisimamia kwa nafasi zao na kuhakisha wananchi wananishi maisha ya raha mustarehe kwani rasilimali za kufanikisha hayo wanazo.

Ukiangalia mambo yanavyokwenda unaanza kupatwa ujasiri wa kuhoji kauli ambazo viongozi wetu wakuu kama raisi ambzo wamekuwa wakizitoa. Ahadi aliyoitoa rais kikwete ya kutowavumilia viongozi au watendaji wababashaji inapaswa kujidhihiri kwasasa ambapo kero za wananchi zimekuwa nyingi bila kuwepo matumaini yoyote ya kutatuliwa hukutukiendelea kushuhudia mbwebwe za wasadizi wake kama mawaziri ambazo kimsingi hazilengi kuwaondolea wananchi matatizo yao.

Huwa napenda kuikariri mara kwa mara kauli ya raisi kikwete aliyiotoa bungeni kwa lugha ya kiingereza nadhani alitka kuonyesha msisitizo na ningependa kuinukuu ‘I might be wearing a smile but I am firm on issues’. Hiyo ni kauli ya raisi kikwete ambayo nadhani ililenga kuwataadharisha wasaidizi wake ili kuonkama ile ya kuwatisha watendaji wake kuwa hatawavumilia pindi watakapoonekana hawatimizi wajibu wao wa kuwatumikia wananchi na kuwaondolea kero zao na hatimaye kufanikisha kauli mbiu ya maisha bora kwa kila mtanzania na sio wana CCM pekee.

Tathmini katika utendaji wa wasaidzi wa raisi kikwete inaacha maswali mengi kuliko majibu. Iko wapi meno ya raisi kikwete? Wasaidizi wake wamekubwa na nini? Wananchi wategemee nini katika kipindi hiki kifupi kilichobaki cha uongozi wake? Je,matatizo au kero za wananchi wetu ni laana isiyoweza kufutika? Tunahitaji nini kuwafanya wasaizi wa viongozi wetu wakuu watimize wajuibu wao?

Ni kwanini rais kikwete uwape fursa wanasiasa,wapinzani wako na wale wasio na mapenzi ya kweli na wewe kuendelea kuhoji uwezo wako ambao kimsingi naamini ni mkubwa kwa makosa ya watendaji au wasaidizi wako ambao kimsingi uwezo wa kuwashughulikia unao ambao una nguvu na baraka za kikatiba. Naamini utakua unaufahamu ule msemo wa wahenga unaohoji busara na ningependa kunukuu

“Busara ya mwenye nyumba kufuga mbwa kisha usiku wa manane anatoka kubweka
mwenyewe”

Ukiangalia muundo wa bajeti zetu unapatwa na ghadhabu kubwa hasa unapoamua kulinganisha fedha zilizotengwa kugharamia matumizi ya kawaida na shughuli za kimaendeleo katika nchi yetu. Sina nia ya kupinga mantiki ya mgawanyo huo ila nakerwa sana na kiasi kikubwa kilichotengwa kuwahudumia wasaidizi hao kama mawziri,wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ambao wengi wao wamekuwa wakishindwa kutimiza wajibu wao katika maenneo yao ya kazi na hivyo kukwamisha juhudi za serikali kuwaletea wananchi maendeleo na kuwaondolea kero zao ambazo zimekuwa zikichangia kudumisha maisha yao kwa kipindi kirefu.

Mimi sioni mantiki ya viongozi wetu wakuu kama rais,waziri mkuu na makamu wa raisi kuendelea kukubali kusulubiwa kama yesu kristo kwa makosa ambayo kimsingi yanachangiwa na wasaidizi wao. Inasikitisha sana pale mtu unapoamua kukadidiso kwa wananchi ni mawaziri gani ambao wao wanadhani wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi unashindwa kupata majina zaid ya kumi(10) katika baraza lenye mawaziri zaidi ya hamsini (50).

Hali ni hiyo hiyo kwa wakuu wa mikoa na wilaya ambao kimsingi ndo wako karibu na wananchi. Kila siku vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti madhila wanayokabiliana nayo wananchi kana kwamba hakuna watu waliopewa majukumu ya kuwasaidia hivyo kuwafanya wajione kama ni yatima katika nchi yao.Kero nyingi ambazo zimekuwa zikiendlea kuwasumbua wananchi kwa kiasi kikubwa zimechangiwa na kutowajibika kwa viongozi au wasaidizi hao ambao wengi wameota pembe na kiburi kitukufu kwani wanajua kuwa hakuna atakayewachukulia hatua.

Vitisho pekee vinavyotolewa na viongozi wakuu dhidi ya wasaidizi au watendaji wababaishaji havitoshi kwani waswahili walishasema sikio la kufa halisikii dawa kwahiyo wakati wa kuwachukulia hatua madhubuti na kali wale wote wanaondelea kuzikalia ofisi za umma na kuendelea kufuja rasilimali za umma bila ya kutimiza wajibu wao wa msingi wa utumishi kwa wananchi umefika na hatpuaswi kusubiri zaidi ya hapa kwani wananchi wanaendela kuteseka.

Hatua aliyochukua raisi kikwete ya kumfukuza mkuu wa mkoa wa mara kanali Enosi mafuru katika sherehe za kufungua hoteli mpya ya kitalii huko Serengeti ili arudi kuwaondelea kero za mapigano wananchi wake ni za kupongezwa lakini hazipaswi kuishia hapo. Wale watumishi ambao wanaonekana kushindwa kutekeleza majukuu yao hawapaswi kufumbiwa macho na kuendelea kulelewa huku wananchi wakiendelea kupoteza maisha na mali zao.

Kwanini fimbo uliyotumia kumchapia mkuu wa wilaya ya karagwe mheshimiwa mnali usiitumie kuwachapia watendaji wengine ambao kwa wakati huu imedhihirika kuwa wako wengi? Kwanini ukubali kujenga hali ya kutoaminika kwa wananchi wako waliokupa dhamana ya kuwatumikia? Kwanini watu waendelee kudhani uamuzi ulioufikia kumuachisha kazi mnali ulikuwa wa kisiasa na sio wa dhamira yako ya kiuongozi? Au unataka wapinzani wako waendelee kupata ya kusema kuwa ulimwachisha kwasababu sio mwanamtandao mwenzako?

Matokeo ya kuendelea kulea uvundo na ugoigoi wa watendaji ni mabaya sana ambayo kimsingi kwa mtu yoyote mwenye akili hapendi kuona yakitokea. Viongozi hawapaswi kusubiri hadi wananchi wakate tamaa na kuanza kujichukulia sheria mkononi au uamuzi wa kuanza kujiongoza wenyewe. Matukio yaliyoshuhudiwa mkoani mbeya katika kipindi cha wiki mbili cha mapambano ya polisi na raia yanapaswa kufungua macho ya watendaji kwani utamaduni wa wananchi kuvamia vituo vya polisi haujazoeleka nchini mwetu na ni ishara ya wananchi kupoteza imani kwa wale waliopewa dhamana za kuwaongoza.

Huku vyama vya upinzani vikjijaribu kuja na mikakati ya kuwahamasisha wananchi kwa kutumia opersheni mbalimbali kama vile operesheni sangara na operesheni sangara mimi namsihi rais kikwete aje na “Opersheni ng’oang’oa” itakayolenga kusafisha na kung’oa mizizi yote ya kutowajibika kwa viongozi wabovu ili kukinusuru chama tawala na kuliokoa taifa lisiangamie kwa mambo ambayo yako ndani ya uwezo wetu.

Huu si wakati wa ushabiki wa kisiasa katika mambo ambayo yanahusu maslahi ya kitaifa na ustawi wa jamii yetu ya kitanzania. Mifumo ya wazi tathmini ya upimaji utendaji kazi wa viongozi wetu na utoaji motisha (Performance based incentives) unapaswa kupewa mkazo ili kuhakikisha rasilimali wanazotumia viongozi wetu zinalingana na tija wanayoileta katika kuwaletea wananchi maendeleo ambao kimsingi ndiyo waajiri wao.

Mungu ibariki Tanzania yetu na viongozi wetu.

2 comments:

iman rahman said...

Nice blog and article, thanks for sharing. However want to statement on few common issues, The website taste is great, the articles is in point of fact excellent.
Obat Vimax

zarena kewat said...

That's what everyone likes. You have a good imagination. Great post thanks you
vimax canada