Tuesday, March 30, 2010

NGUVU YA MALUMBANO YA SERIKALI NA MENGI IELEKEZWE KWENYE VITA DHIDI YA MAUAJI YA ALBINO

Jukumu moja kubwa kwa serikali yoyote ile duniani ni kusimamia uhai wa watu wake na mali zao.Haiingia akilini kuona serikali makini ikitelekeza wajibu wake huu mkubwa na kuanza kujihusisha katika malumbano yasiyo na tija kwa wananchi wake na kuwaacha makumi kwa mamia ya raia wake wakipoteza uhai ambao ni haki yao ya msingi na ambao serikali iliapa kuulinda na kuutetea.

Nadiriki kuamini kuwa kauli ya serikali iliyotolewa na waziri wa mambo ya ndani ya nchi mheshimiwa Lawrence masha dhidi ya mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP mzee Reginald mengi ya kumpa siku saba athibitishe madai yake aliyotoa kuhusu waziri mmoja kijana anyesuka njama za kumhujumu katika shughuli zake za kibishara ni ushahidi mwinginbe ulio wazi kuwa serikali yetu imekosa agenda muhimu za kusimamia.

Sitaki kuamini madai yaliyotolewa na mzee mengi yanageuka kua agenda muhimu kwa serikali makini. Serikali isiyo na agenda mara nyingi kama si zote imekua ikitapatapa kwa kila jambo linaloibuka hata wakati mwingine likiwa halina maana wala tija katika ustawi wa kijamii au kiuchumi wa jamii husika.Sitaki kuaamini kuwa madai ya mengi yaliyoibiliwa hivi karibuni yanapaswa kupewa nguvu kubwa kama inavyoelekea kupewa hivi sasa na wadau wa serikali na vyama vya siasa ambao mwisho wake ni kuendelea kuwagawa wananchi na kuwayumbisha na hatimaye kutumbukia katika mijadala isiyo na maana wala heri kwa taifa letu.

Waziri Masha ni mdau mkuu na muhimu na aliyepewa dhamana katika kusimamia usalama wa raia na mali zao na anapaswa kubuni mikakati na miongozo katika vita dhidi ya ukatili unaoendela kwa watanzania wenzetu wenye ulemavu wa ngozi wanaojulikana kwa sasa kama Maalbino na siyo kujitumbukiza katika malumbano yanayoelekea kuchafua roho zetu na kusahaju jukumu muhimu alilopewa la kusimamia uhai na usalama wa raia walio wengi haswa maalbino walio katika hatari ya kuotokomea

Jamii hii ya watanzania hawa walemavu wa ngozi wamepoteza matumaini ya kuishi na hawana uhakika kama wataiona kesho kwani maisha yao siku zote yako hatarini.Nguvu zao za kujilinda dhidi ya ukatili huu ni dhaifu ukilinganisha na za maadui wao ambao imekuja kubainika kuwa baadhi yao ni askari ambao kimsingi walipaswa kuwalinda.

Serikali inatoa siku saba kwa mtu mmoja kuthibitisha madai ambayo mwisho wake utaishia kule kule kwa malimbano ya awali kati mwenyekiti huyo na mbunge wa mkuranga mheshimiwa Adam malima na huku maalbino wakiendelea kupoteza maisha bila mtetezi wa kweli na haki yao ya msingi ya uhai ikiendelea kuchezewa danadana.

Waganga wa jadi wanaendelea kutamalaki na kuchochea mauaji ya watanzania wenzetu wasio na hatia huku serikali ikijihusisha katika malumbano yasiyo na msingi na kusahau agenda zake za kutetea maisha ya wananchi wake na kuandaa mazingira salama ya wao kujishughulisha na kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Serikali inaanza kupoteza muelekeo na kubaki na agenda moja kila kukicha ya kujisafisha dhidi ya kashfa na madhambi yanayowaandama watendaji wake mmoja mmoja au serikali nzima kwa ujumla.Nani kasema mengi ni muhimu kuliko maisha ya albino wanaopteza maisha kila kukicha?Nani kasema waziri mtuhumiwa ni muhimu kuliko maisha ya ndugu zetu hawa wanaoangamia bila sababu?Nani kasema usafi wa serikali machoni mwa watanzania ni muhimu kuliko uhai wa wananchi wake?

Vyombo vya habari navyo vinaelekea kupotezwa muelekeo na kujikuta vinajinasa katika mtego wa malumbano na kupoteza dhima nzima ya habari na umuhimu wake katika kupinga vita maovu kama haya dhidi ya watanzania wenzetu wenye ulemavu wa ngozi.Maisha ya maalbino yanafanywa kama ni mambo yasiyo na msingi na kuendekeza malumbano ya kisiasa ambayo ni wazi kuwa hayana tija katika maisha ya watanzania na katika uhai wa ndugu zetu hawa.

Juzi mlemavu mwingine wa ngozi wa kijiji cha Nkindwabye willayani Bariadi ameuawa kikatili kwa wauaji kutoweka na kichwa na miguu yake yote miwili.Hakika maisha ya ndugu zetu hawa yanaonekana hayana thamani na nguvu inayoelekezwa kuyalinda nachelea kusema kuwa inatosha na yenye nia thabiti ya kuyatokemeza kabisa.

Siku saba alizopewa mzee mengi kama nilivyodokeza hapo juu zingepaswa kuelekezwa katika kuokoa maisha ya ndugu zetu hawa ambao kimsingi wamebakia bila mtetezi wa kuaminika na mwenye nia ya kuwafanya waishi maisha ya amani na utilivu wa moyo kwa wakati wote ule kwani serikali inasahau jukumu lake na vyombo vya habari navyo halikadhalika.

Serikali siku zote imekua ikiaminika kuwa na mkono mrefu ambao una nguvu ya kuwafuata wale wote wanaojihusisha na uovu na kuwaleta katika vyombo vya sheria.Kutumia nguvu hiyo kwa mtu mmoja kwa lengo la kujisafisha machoni mwa mwananchi huku makumi ya raia wengine walemavu wakiendelea kupoteza maisha yao ni aina nyingine ya ubabaishaji.

Wizara ya mambo ya ndani ambayo waziri masha anaisimamia inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupiga vita unyama huu ambao unaendelea kulitia doa taifa letu ambalo siku zote tumekua tukijisifia kuwa kinara wa amani na utulivu.Si busara kwa seriakli kuendelea kutumia nguvu kubwa kwa mtu mmoja na huku tukiacha mamia ya wananchi wetu wakiangamia.

Malumbano haya hayana muelekeo mwema kwaiyo ni vyema wadau wote washirikiane na waelekeze nguvu zao katika kuokoa maisha ya watanzania wenzetu.Nguvu kubwa ya kutumia vyombo vya habari katika kuchafuana na kujisafisha ni busara ikaelekezwa katika vita ya kupinga mauaji ya maalbino.
gasper_materu@yahoo.ca

1 comment:

myslot said...

หนังออนไลน์สนุกต้อง Alita: Battle Angel อลิตา แบทเทิล แองเจิ้ล (2019) ดูหนังเรื่องนี้ที่นี่เว็บหนังฟรี

https://www.doonung1234.com/